1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasiwasi na taharuki vimetanda mjini Uvira DRC

10 Desemba 2025

Wasiwasi na taharuki vimetanda katika mji wa Uvira, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, kufuatia mapigano kati ya waasi wa AFC/M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, dhidi ya jeshi la Kongo.

https://p.dw.com/p/553Vy
DR Congo Goma 2025 | Waasi wa M23 wakiandikisha wafuwasi wapya baada ya kupata maeneo.
Waasi wa M23 wakiandikisha wafuwasi wapya baada ya kudhibiti maeneo.Picha: Michel Lunanga/AFP/Getty Images

Hali ya wasiwasi na taharuki vimetanda katika mji wa Uvira, Mashariki mwa  Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo, kufuatia mapigano kati ya waasi wa AFC/M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, dhidi ya jeshi la Kongo linalosaidiwa na jeshi la Burundi na wapiganaji wa kujitolea wa kundi la Wazalendo.

Hadi asubuhi ya leo waasi wa AFC/M23 hawakuwa wameingia Uvira, licha ya kwamba idadi kubwa ya wanajeshi wa FARDC kuonekana ikiondoka mjini humo.

Kupitia simu yake ya mkononi, Jean-Luc, mkazi wa Uvira aliyekuwa akitembea mitaani, aliwahakikishia wananchi wenzake kwamba hadi asubuhi wapiganaji wa AFC/M23 bado hawajafika mjini. Baada ya usiku wenye taharuki uliosheheni milio ya risasi na visa vya uporaji, Patrick pia aliamka na kujitokeza barabarani ili kujionea hali halisi.

Taarifa ya waasi wa AFC/M23 kuingia Uvira

Maisha ya soko licha ya kitisho cha waasi wa M23
Maisha ya sokoni mjini Uvira licha ya kitisho cha waasi wa M23.Picha: AFP

Hadi usiku wa manane, taarifa zisizohakikiwa zilienea kwenye mitandao ya kijamii kwamba AFC/M23 tayari wameingia Uvira. Hata hivyo, vyanzo vya usalama vya FARDC vilikanusha, ingawa wanajeshi kadhaa na wapiganaji wa Wazalendo walionekana Jumanne wakielekea kijiji cha Makobola kusini mwa Uvira, na wengine wakijaribu kusafiri kuelekea Kalemie. Jeshi la Kongo linasisitiza kuwa linaendelea kuwapo Uvira.

Mashahidi, hata hivyo, wanadai kuwa waasi wa AFC/M23 wako karibu mno na jiji hilo, wakisemekana kuonekana maeneo ya kati ya Kiliba na vitongoji vya karibu na Uvira. Ikumbukwe kwamba wakati wa kutekwa kwa maeneo yenye wakaazi wengi kama Sake na Bukavu mapema mwaka huu, wanajeshi wa Kongo na Wazalendo walijiondoa kabla ya AFC/M23 kuingia, jambo lililozua sintofahamu kubwa.

Umuhimu wa mji wa Uvira

Mji wa Uvira una umuhimu wa kipekee, ukitazamana kabisaa na mji mkuu wa Burundi Bujumbura, hii ikimaanisha kuwa kuanguka kwa Uvira mkononi mwa AFC/M23, kunauweka katika mashaka makubwa usalama wa Burundi.

Katika taarifa iliyotolewa leo asubuhi, Rwanda imeshutumu majeshi ya Kongo na Burundi kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ya Washington, ikisema hali hiyo inaendeleza mateso ya wakaazi wa Mashariki mwa Kongo na kuibua tishio la usalama katika mpaka wake wa magharibi.

DW, Bukavu