Hali ya vyombo vya habari katika mataifa ya Latin Amerika inatatanisha. | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali ya vyombo vya habari katika mataifa ya Latin Amerika inatatanisha.

Watu wameanza kulumbana katika mataifa ya Amerika ya kusini, kwasababu ya uamuzi wa serikali ya Venezuela kutokipatia leseni tena ya utangazaji , kituo maarufu cha televisheni nchini humo cha RCTV.

Marais watatu wa zamani wa Panama , Mireya Moscoso, Guillermo Endara na Ernesto Perez-Balladares, wanapanga kuushawishi umoja wa mataifa ya latin Amerika OAS, kulizungumzia suala hilo katika baraza lake kuu katika mkutano wake mwishoni mwa juma lijalo.

Na rais wa Peru Alan Garcia amesema , kutokana na uamuzi wa kutoipatia tena leseni ya utangazaji RCTV, ambayo imekuwa ikitangaza tangu mwaka 1956, nchini Peru kitu kama hicho hakiwezi kutokea.

Watu wengi nchini Venezuela wanadai kuwa RCTV , yaani radio Caracas Televishen, imejichimbia kaburi lake yenyewe kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya serikali ya rais Hugo Chavez, ambao umekwenda umbali wa kuunga mkono mapinduzi ya Aprili 2002 ambayo kwa muda yaliuangusha utawala wa rais Chavez.

Katika nchi jirani ya Colombia , ambayo imekuwa ikidhibitiwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda karibu nusu karne, mwandishi habari Juan Gossain wa kituo cha radio cha RCN amesema katika mahojiano na rais Alvaro Uribe, kuwa matamshi yako ya kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari , yanapelekea kufikiria kwa mfano kuwa , hungeweza kufuta leseni ya utangazaji ya kituo cha RCTV.

Ambapo rais alijibu kuwa nisingeweza kufanya hivyo kwa mtu yeyote. Ama waache watumie haki yao ya uandishi habari hata bila ya kuwa na leseni, wanaweza kusema watakavyo, wanaweza kufanya chochote wakati watakao.

Lakini rais huyo mwenye kuelemea bawa la kulia , Uribe hawezi kufunga kituo chochote cha matangazo kwa sababu finyu kama hiyo , kwa kuwa hakuna kitu kama hicho nchini mwake, ukilinganisha na Venezuela, ambako vituo vingi vinavyomilikiwa na watu binafsi vinapingana na serikali wazi kabisa.

Hapo mapema , hata hivyo Oktoba 2004, utawala wa rais Uribe ulikifunga kituo cha matangazo ya radio na televisheni cha Inravision, ambacho kilikuwa kinatangaza katika vituo vitatu. Matangazo yake yalikuwa ni pamoja na elimu, na utamaduni, vipindi vya kila siku vya mahojiano juu ya harakati za kijamii, pamoja na makala ambazo zilikuwa zinaonekana kuwa tofauti na mtazamo wa serikali.

Rais huyo alitoa tangazo lake kuhusu Inravision siku ya Jumatatu na Alhamis iliyofuata polisi waliingia katika kituo hicho na kuwaondoa wafanyakazi siku hiyo hiyo.

Nchini Honduras, wakati huo huo , rais Manuel Zelaya ameamuru televisheni zote pamoja na radio kutangaza vipindi kumi kila siku vya saa moja wakati wenye watazamaji wengi, kuanzia Jumatatu, kupambana na kile alichosema kuwa ni upotoshaji habari, kuhusiana na utawala wake unaotolewa na vyombo vya habari.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Juan Ramon Martinez ameliambia shirika la habari la IPS kuwa uamuzi huo ni pigo kwa uhuru wa kujieleza na kwamba hata jeshi halikuwa linaendea kinyume haki hizo kama serikali za sasa zinavyofanya.

Nchini Nicaragua , kituo cha mwisho kupoteza leseni yake ya utangazaji kutokana na sababu za kisiasa kilikuwa ni La Poderosa radio mwaka 2002, wakati wa utawala wa Enrique Bolanos, wakati vyombo vya utangazaji vya kituo hicho vilipokamatwa kinyume na

utaratibu wa kisheria.

 • Tarehe 30.05.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHDX
 • Tarehe 30.05.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHDX

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com