Hali ya rais Hugo Chavez iko imara, asema makamu wa urais Venezuela | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ya rais Hugo Chavez iko imara, asema makamu wa urais Venezuela

Makamu wa rais nchini Venezuela Nicolas Maduro amesema rais wa nchi hiyo Hugo Chavez amepata fahamu na kutambua kinachoendelea baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na rais huyo kuugua saratani

Makamu wa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro

Makamu wa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro

Maduro ametupilia mbali wasiwasi uliokuwepo juu ya hali ya kiafya ya rais Chavez wakati huu ambapo anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais katika siku kadhaa zijazo.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari hapo jana, Makamu huyo wa urais, Nicolas Maduro, amesema amemtembelea Hugo Chavez hospitalini nchini Cuba anakopokea matibabu, na kusalimiana kwa mkono huku Chavez akionekana mwenye nguvu kabisa. Chavez anatarajiwa kuapishwa tarehe 10 mwezi huu kama rais wa Venezuela kwa kipindi cha miaka sita ijayo.

Rais wa Venezuela Hugo Chavez

Rais wa Venezuela Hugo Chavez

Lakini kutokana na hali yake kiafya kutokuwa ya kuridhisha, mwelekeo wa kisiasa nchini humo umekuwa wa wasiwasi mkubwa. Makamu wa rais Maduro sasa ameunyoshea kidole cha lawama upande wa mrengo wa kulia na baadhi ya vyombo vya habari nchini Venezuela kwa kutilia chumvi habari juu ya afya ya Chavez.

Amesema rais anakabiliana na maradhi yake kwa hadhi kubwa na matumaini. Chavez anayeugua ugonjwa wa saratani alifanyiwa upasuaji wa nne Disemba 11 mjini Havanna. Hadi sasa bado haijabainika rais huyo wa Venezuela anaugua saratani ya aina gani tangu alipogundulika kuugua ugonjwa huo mwezi Juni mwaka wa 2011.

Hali ya kiafya ya rais Chavez yazidi kuzua maswala mengi

Chavez anayeiongoza nchi hiyo tangu mwaka wa 1999, kurejea kwake hospitalini mara kwa mara kumezua maswali ya iwapo anaweza kweli kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mwengine. Hata hivyo mwaka uliopita Chavez alimchagua Maduro kuwa mrithi wake na kuwahimiza raia wa Venezuela kumchagua awaongoze iwapo uchaguzi mpya utaitishwa.

Baadhi ya wakaazi wa Venezuela wakati wa uchaguzi uliopita

Baadhi ya wakaazi wa Venezuela wakati wa uchaguzi uliopita

Kulingana na katiba ya Venezuela uchaguzi mpya unaweza kuitishwa kati ya siku 30 iwapo rais atafariki au kutokuwa katika hali nzuri ya kuongoza nchi.

Hata hivyo kumekuwa na habari mbali mbali katika mitandao ya kijamii kama twitter inayosema rais Chavez amewekwa katika mashini ya kumsaidia kuishi na wengine kusema kuwa tayari rais huyo ameshafariki. Kwa upande wake makamu wa rais ametupilia mbali taarifa hizo na kusema wanaozieneza ni wale walio na chuki na roho mbaya kwa rais Chavez.

Raia wa Venezuela waliukaribisha mwaka wa 2013 wakijiuliza maswali mengi juu ya namna maisha yatakavyokuwa bila ya rais wao Hugo Chavez. Baadhi ya sherehe za mwaka mpya zilisimamishwa ili kutoa nafasi ya kufanyika maombi kwa rais huyo. Elisabeth Torres raia wa nchi hiyo amesema familia yake ilienda kulala mapema usiku wa mkesha wa mwaka mpya na pia kumuombea Chavez apate nafuu. Torres alisema wanamkosa na kumpenda sana rais wao.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com