1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kisiasa nchini Ivory Coast inazidi kuwa tete

18 Februari 2010

Waziri mkuu Guillaume Soro kuitangaza serikali wiki hii huku jeshi likiwaonya wapinzani wanaoandamana

https://p.dw.com/p/M4YN
Maandamano katika mji wa AbidjanPicha: AP
Maelfu ya watu walijitokeza jana kuandamana katika sehemu mbali mbali nchini Ivory Coast kupinga uamuzi wa rais Laurent Gbagbo wa kuivunja serikali pamoja na tume ya uchaguzi. Hatua hiyo ya Rais Gbagbo imeibua hali ya wasiwasi katika taifa hilo pamoja na hofu kwamba itachelewesha tena hatua ya kufanyika uchaguzi wa rais uliokuwa umepangwa kufanyika mapema mwezi wa Marchi. Uamuzi wa Rais Gbagbo, uliokuja baada ya mvutano na tume ya uchaguzi kuhusiana na daftari la wapiga kura, unaelekea utasababisha kuchelewesha tena uchaguzi wa rais wa mwezi Marchi. Mvutano wa kisiasa umeongezeka makali huku upinzani ukiandaa maandamano makubwa zaidi na kuongeza kitisho cha kuzuka kwa machafuko katika taifa hilo linalozalisha kwa wingi zao la kakao duniani. Hata hivyo, hadi sasa maaandamano yaliyofanyika yamekuwa ya utulivu ikiwa ni pamoja na hapo jana yaliyofanyika katika sehemu kadhaa za taifa hilo. Katika mji mkuu wa Abidjan waandamanaji waliliteka nyara basi moja la kampuni ya usafiri ya taifa na kulitia moto. Maandamano hayo pia yamefanyika katika miji ya eneo la kati ya Daoukro,Dimbokro na M'bahiakro ambapo waandamanaji walifunga barabara na kuwasha moto matairi. Kutokana na hali hiyo tete iliyojitokeza, mkuu wa jeshi nchini humo, Jenerali Phillipe Mangou, amewaambia waandishi wa habari katika mji wa Yamoussoukro kuwa vikosi vya usalama vitailinda serikali dhidi ya machafuko yoyote ya raia. Rais wa Burkina Faso, Blaise Campaore, ambaye ni mpatanishi katika mzozo wa Ivory Coast amemtolea mwito rais Gbagbo kuanzisha tena shughuli zilizokwama za maandalizi ya 5 uchaguzi.
Laurent Gbagbo
Rais Gbagbo aliivunja serikali na tume ya uchaguzi na kuzusha mvutano wa kisiasa unaoweza kuchelewesha uchaguzi mkuu wa Marchi.Picha: AP
Akizungumzia kuhusu hali hiyo tete iliyojitokeza Ivory Coast, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini humo, kutoka shirika la kimataifa linashughulikia mizozo, Renaldo Depagna amesema- ''Utaratibu wa uchaguzi umesitishwa kwa sasa na utaanza, pengin, serikali mpya ikitangazwa, na hasa tume mpya na huru ya uchaguzi ikiundwa. Lakini yote haya yanaweza kuchukua wiki kadhaa. Serikali mpya iliyokuwa itangazwe jana imeahirishwa kuundwa na vyombo vya habari vinasema pengine itatangazwa mwishoni mwa wiki.Yote haya yanachelewesha kutangazwa tume mpya ya uchaguzi ambayo Laurent Gbagbo amemtaka waziri mkuu wake aiunde'' Waziri mkuu Guillaume Soro anatarajiwa wiki hii kuitangaza serikali ingawa haijawa bayana ni lini tume ya uchaguzi itatangazwa. Waandamanaji wanadai kwamba wamechoshwa na rais Gbagbo wanayemtaja kama ni dikteta pamoja na utawala wake. Uchaguzi wa Ivory Coast umecheleweshwa tangu mwaka 2005. Lakini mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Renaldo, anasema waziri mkuu huyo anakabiliwa na changamoto kubwa katika kuunda serikali pamoja na tume ya uchaguzi. ''Ni shida kwa waziri mkuu kwa sababu, kimsingi, anabidi afuate msimamo wa usimamizi, anabidi ahakikishe utaratibu wa uchaguzi unaheshimiwa na kufanyika kama ilivyopangwa. Ikiwa kila kitu kitapita kama ilivyopangwa, yeye pia ataweza kujihakikishia mustakabal mwema wa maisha yake ya kisiasa'' Miito kutoka jumuiya mbali mbali imetolewa ya kulitaka taifa hilo liutatue mgogoro huu, ukiwemo wito wa Jumuiya kiuchumi ya nchi za magharibi mwa Afrika, ECOWAS. Kwa upande mwingine, mzozo huo pia umetatiza shughuli za sekta ya Kakao ambayo inatoa asilimia 40 ya mahitaji ya dunia ya zao hilo. Mwandishi Saumu Mwasimba/RTRE Mhariri Othman Miraji