Hali ya kisiasa Israel baada ya waziri mkuu Olmert kutangaza ataacha madaraka. | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ya kisiasa Israel baada ya waziri mkuu Olmert kutangaza ataacha madaraka.

Chama cha kadima kumchagua kiongozi mpya mwezi ujao

Bibi Tzipi Livni anayetajwa kuwa nafasi nzuri ya kushika uongozi wa Kadima baada ya Bw Olmert

Bibi Tzipi Livni anayetajwa kuwa nafasi nzuri ya kushika uongozi wa Kadima baada ya Bw Olmert

Nchini Israel wakati Waziri mkuu Ehud Olmert akiwa ametangaza kwamba atan´gatuka madarakani pale atakapochaguliwa kiongozi mpya wa chama chake cha Kadima mwezi Septemba, wengi miongoni mwa waisraili wanaamini uamuzi wake ni wa busara.

Hata hivyo utafiti wa maoni ya wapiga kura unaashiria kinayangayiro kikubwa kati ya wanasiasa wawili wa vyama tafauti pale uchaguzi mkuu utakapoitishwa baada ya Olmert kuondoka madarakani.

Wanasiasa hao wawili ni Kiongozi wa chama cha Likud cha mrengo wa kulia waziri mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu na waziri wa mambo ya nchi za nje Tzipi Livni ikiwa chama chake cha Kadima kitamchagua yeye kuwa mrithi wa waziri mkuu wa sasa Ehud Olmert.

Utafiti wa magazeti yote matatu makubwa nchini Israel leo umeonyesha kuwa Bibi Livni anaongoza katika kuwania nafasi ya kuchukua uongozi wa chama cha Kadima katika uchaguzi wa Septemba 17.

Kwa muda sasa utafiti pia umekua ukiashiria kwamba chama cha Bw Netanyahu cha Likud,kitashinda uchaguzi wa bunge dhidi ya Kadima, lakini magazeti mawili kati ya matatu yametabiri kwamba kutakua na ushindani mkali ikiwa bibi Livni atachaguliwa kuwa kiongozi wa Kadima.

Mpinzani mkubwa wa Bibi Livni katika kuwania uongozi wa chama ni Waziri wa uchukuzi Shaul Mofaz anayeaminiwa kuwa mfuasi wa Olmert. Pamoja na hayo mtazamo wa wengi ni kuwa Mofaz hatokua na heba ya kuwavutia wapiga kura hasa katika wakati huu hata hivyo Bw Netanyahu anayekosoa msimamo wa Olmert juu ya mazungumzo na wapalestina na pia na Syria, ndiye anayeonekana kuwa mwanasiasa maarufu katika kugombea wadhifa wa waziri mkuu.

Kwa upande mwengine mtazamo jumla wa waisraili ni kwamba,uamuzi wa Bw Olmert kuwa ataacha madaraka ya Uwaziri mkuu, ni uamuzi barabara. Utafiti umeonyesha 91 asili mia wameliunga mkono tangazo hilo la Bw Olmert Jumatano usiku.

Wachambuzi wanasema, iwe ni Likud au Kadima, lakini turufu inawezekana ikawa kwa chama cha Leba, kwani yeyote atakayeshinda uchaguzi atalazimika kuunda serikali ya mseto . Chama cha Leba kinaweza kuwa karibu zaidi na Kadima kuliko na Likud chini ya uongozi wa Netanyahu.

Wakati huo huo Waziri mkuu Olmert alihojiwa tena na polisi leo kuhusiana na madai ya kuhusika katika vitendo vya rushwa, chanzo cha wito wa kumtaka ajiuzulu.

Binafsi alipotoa tangazo la kuwa ataacha madaraka Septemba, aliungama kwamba kisa hicho umekua mzigo kwa familia yake na kusema " Nimefanya makosa na ninasikitika kwa hilo."

Polisi ilisema masuali yanayomkabili Bw Olmert huenda yakawa juu ya madai kwamba alipokea fedha kwa ajili ya uchaguzi na mambo mengine kutoka kwa tajiri mmoja wa Kimarekani na kuwa aliwasilisha stakabadhi kadhaa kwa safari zile zile alizofanya nchi za nje, jambo linalochukuliwa kuwa ni udanganyifu.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com