1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hewa barani Ulaya yaanza kurejea katika hali ya kawaida, huku ikiwa imesababisha vifo vya zaidi ya watu 80.

22 Desemba 2009

Ni kutokana na baridi kali iliyoambatana na theluji.

https://p.dw.com/p/LAZc
Baridi kali na theluji ikiwa imetanda, ambavyo vilisababisha usafiri wa treni kusitishwa katika baadhi ya maeneo barani Ulaya.Picha: AP

Wakati hali ya hewa katika sehemu kubwa barani Ulaya ikiwa inaanza kupunguza makali yake, baridi kali, upepo na theluji vilivyolikumba bara hili kwa siku kadhaa vimeacha maafa makubwa katika sehemu mbalimbali barani humu.

Idadi ya vifo vilivyosababisha na hali hiyo ya baridi kali na theluji katika pande mbalimbali barani ulaya, sasa imefikia kiasi ya watu 80, wakati mtafaruku wa usafiri ukisababisha hasira kali kwa wasafiri, kutokana na kampuni ya treni za mwendokasi ya Eurostar kushindwa kutoa huduma kwa siku tatu.

Maelfu kwa maelfu ya wasafiri walikwama vituo vya London na Paris kutokana na kufutwa kwa safari, huku safari za ndege nazo zilifutwa barani humu kutokana na viwanja kujaa theluji, ajali za barabarani na kukatika kwa umeme, vikizidisha machungu ya hali ya hewa yenye baridi kali.

Treni moja katika mji mkuu wa Croatia ya Zagreb iligonga eneo la hifadhi na kujeruhi watu 52.

Televisheni ya nchi hiyo imesema wachunguzi nchini humo wameilaumu hali ya hewa yenye baridi kali iliyo chini ya kipimo cha nyuzijoto 10, na theluji nyingi kuwa chanzo kilichosababisha breki za treni hiyo kushindwa kukamata.

Nchini Poland maafisa wa nchi hiyo wamesema watu 42, wengi wao wakiwa hawana makazi wamekufa kutokana na baridi kali iliyodumu kwa siku tatu mfululizo, ambayo ilikuwa chini ya nyuzi joto 4.

Ukraine imeripoti vifo vya watu 27 wakati watu sita wamekufa nchini Ujerumani kutokana ajali za barabarani, zilizosababishwa na theluji kujaa kwenye barabara hizo, huku watu watatu wakiripotiwa kufa nchini Austria.

Safari nyingi za ndege zilifutwa nchini Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Ureno na Uhispania, na barabara kuu za barani zilifungwa ambapo katika baadhi ya mikoa theluji ilifikia kiasi ya sentimita 50 kutoka usawa wa ardhi.

Matatizo ya usafiri wa treni yamesababisha Waziri wa Usafirishaji wa Ufaransa kuagiza kufanyike uchunguzi wa kina juu ya tatizo la kukwama kwa treni hizo.

Hata hivyo baada ya msukosuko huo uliosababisha wasafiri zaidi ya 2000 kukwama tangu Ijumaa ya wiki liyopita, na zaidi ya maelfu wengine wakizichelewa treni walizopaswa kusafiri nazo kutokana na kufutwa au kubadilishwa ratiba, kampuni ya Eurostar imetangaza kuanza kwa safari chache hii leo, kutokana na hali ya hewa kuanza kurejea katika hali yake ya kawaida.

Treni mbili zilipangwa kuanza kazi alfajiri ya leo, moja ikitokea mjini Paris, na nyingine ikianza safari kutoka mjini London.

Sakata la treni hizi lilianza Jumamosi ya wiki iliyopita, pale treni za Eurostar zilipokwama chini ya handaki kwa zaidi ya saa 15, na kusababisha kusitishwa kwa huduma za kampuni hiyo.

Kusitishwa kwa safari za treni hizo mwishoni mwa wiki iliyopita kuliathiri takribani watu 59,000, miongoni mwao ni familia nyingi na watoto, ambao walikuwa wakisafiri kwa ajili ya kwenda kusherehekea sikukuu ya krismas na jamaa zao.

Mwandishi:Lazaro Matalange/DAP/AFP

Mhariri:Othman Miraji