Hali ya Hatari yatangazwa Ufaransa baada ya mashambulizi ya kigaidi | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali ya Hatari yatangazwa Ufaransa baada ya mashambulizi ya kigaidi

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza hali ya hatari na kuagiza mipaka yote nchini humo kufungwa baada ya misururu ya mashambulizi yaliowalenga vijana katika mikahawa kadhaa, kusababisha zaidi ya watu 120 kuuwawa

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Waziri wa ndani Bernard Cazeneuve na Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls, wakizungumza na waandishi habari mjini Paris

Rais wa Ufaransa Francois Hollande, Waziri wa ndani Bernard Cazeneuve na Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls, wakizungumza na waandishi habari mjini Paris

Rais Hollande ameapa Ufaransa itasimama imara dhidi ya kile alichokiita ugaidi. Shambulizi kubwa lilitokea katika ukumbi wa maonyesho uliokuwa na Bendi ya Rock kutoka Marekani ambapo watu kadhaa walishikiliwa mateka kisha baadaye washambuliaji wakawatupia mabomu mateka hao. Aidha polisi waliovamia eneo hilo wanasemekana kufanikiwa kuwaua washambuliaji zaidi ya watatu.

Kwengineko maafisa wa polisi wamesema watu wengine 11 wameuwawa katika hoteli ya Le Carillon, na Bataclan baada ya washambuliaji kuanza kumimina risasi katika eneo hilo. Hoteli hizo mbili ziko karibu na jengo la ofisi za Charlie Hebdo zilizoshambuliwa na magaidi mwaka huu. Vile vile watu wengine watatu waliuwawa baada ya bomu kuripuka nje ya uwanja wa mpira wa Stade de France, mjini humo, wakati mabingwa wa kombe la dunia Ujerumani walipokuwa wanacheza na wenyeji wa fainali za mwakani za kombe la mataifa ya Ulaya, Ufaransa.

Watu waliojeruhiwa wakikimbilia eneo salama baada ya mashambulizi ya kigaidi

Watu waliojeruhiwa wakikimbilia eneo salama baada ya mashambulizi ya kigaidi

Kulingana na mwandishi wa chombo cha habari cha Associated Press ndani ya uwanja huo wa mpira, milipuko miwili ilisikika ndani ya uwanja huo, kisha ikafuatiwa na milio ya gari za kubebea wagonjwa na baadaye helikopta ikaonekana ikizunguka juu ya uwanja huo. Hakuna kundi lolote lililojitokeza kudai kuhusika na shambulizi hilo lakini wapiganaji wa jihadi kupitia mtandao wao wa kijamii wa Twitter wamepongeza mashambulizi hayo nchini Ufaransa.

"Hili ni tukio la kutisha lililotukumba tena, tunajua limetokea wapi, tunawajua wahalifu ni kina nani, hawa magaidi ni nani," alisema rais Francois Hollande. Shambulizi hili linatokea wakati Ufaransa ikiwa imeimarisha usalama kuelekea mkutano mkubwa wa tabia nchi unaoanza ndani ya wiki mbili zijazo. Rais huyo amefuta safari yake nchini Uturuki, kuhudhuria mkutano unaoanza Jumapili (15.11.2015) wa viongozi kutoka nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiviwanda duniani zinazojulikana kama G20 kujadili mgogoro wa Syria, Mgogoro wa wakimbizi na mabadiliko ya tabia nchi.

Nchi kadhaa zakimataifa zatoa hisia zao juu ya shambulizi la kigaidi, Ufaransa

Huku hayo yakiarifiwa ulimwengu wa kimataifa umetoa hisia zake juu ya shzambulizi hilo. Rais wa Marekani Barrack Obama akizungumza na waandishi habari mjini Washington ameliita shambulizi hilo kama tukio la kikatili linalolega kuwatishia raia wasio na hatia na kuapa kufanya kila awezalo kuhakikisha waliotenda uhalifu huo wanawajibishwa.

Rais wa Marekani Barrack Obama

Rais wa Marekani Barrack Obama

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema amesikitishwa na picha anazoziona nchini Ufaransa. Katika taarifa yake Merkel amesema yuko pamoja na familia ya waathiriwa wa mkasa huo.

Taasisi tatu za Umoja wa Ulaya zimetoa taarifa ya pamoja kulaani shambulizi dhidi ya Ufaransa na kuliita kuwa ni "kitendo kisichokubalika" huku wakionyesha mshikamano na Ufaransa. Wawakilishi kutoka Baraza la Umoja wa Ulaya, Bunge la Ulaya na Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya walikuwa katika mkutano wa mazungumzo ya bajeti wakati walipopata habari kuhusu shambulizi hilo.

Aidha Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker amemuandikia barua rais wa Ufaransa Francois Hollande kuelezea masikitiko yake ya kuiona Ufaransa ikikumbwa na shambulizi la kutisha la kigaidi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kwa upande mwengine Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon pia amelaani shambulizi hilo na kutoa salamu zake za rambi rambi kwa familia za waathiriwa na kuwatakia afueni ya haraka wale waliojeruhiwa.

Ban Ki Moon amesema anasimama pamoja na serikali ya Ufaransa na watu wa Ufaransa. Uingereza, Israel, Saudi Arabia, na Uturuki ni miongoni mwa nchi zilizolaani shambulizi hilo la kigaidi nchini Ufaransa.

Jeshi la Ufaransa linawashambulia wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Syria na Iraq pamoja na kupambana na wanamgambo walio na itikadi kali za kidini barani Afrika na makundi hayo awali yamekuwa yakitoa vitisho kwa Ufaransa. Nchi hiyo imekuwa na wasiwasi juu ya kitisho kinacholetwa na raia kadhaa wa Ufaransa walio na itikadi kali za kidini waliosafiri nchini Syria na kurejea nyumbani na taaluma ya kushambulia na kusababisha machafuko.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com