1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yapeleka polisi zaidi ya 2000 Jerusalem

Iddi Ssessanga
18 Mei 2023

Israel imepeleka askari polisi zaidi ya 2000 kutoa ulinzi kwa Wayahudi wenye misimamo mikali wanaoandama katika mji mkongwe wa Jerusalem, kuadhimisha kumbukumbu ya kutekwa kwa mji huo na Israel mnamo mwaka 1967.

https://p.dw.com/p/4RXUw
Israel Jerusalem: Zusammenstöße in Al-Aqsa, Hamas
Picha: Mahmoud Illean/AP Photo/picture alliance

Mamlaka zinasema usalama ulioimarishwa ni juhudi iliyokusudiwa kuhakikisha maandamano hayo yanapita bila vurugu zozote.

Polisi wameamua kuruhusu maelfu ya waandamanaji kutumia njia ya jadi kupitia Lango la Damascus la mji huo mkongwe, licha ya kuongezeka kwa vurugu kati ya Israel na Wapalestina katika kipindi cha mwaka uliopita, na mapigano makali kati ya Israel na wapiganaji wa Kipalestina mjini Gaza wiki iliyopita.

Maandamano hayo yanatazamwa kama hatua ya uchokozi kwa Wapalestina, ambao wanalazimika kufunga maduka yao na wanapigwa marufuku kuingia katika kitovu cha kijamii cha Lango la Damascus ili kuwapisha waandamanaji.

Istael | Zusammenstöße in Jerusalem
Israel imepeleka askari polisi zaidi ya 2000 kulinda usalama katika eneo la mji mkongwe la Jerusalem yanakopangwa maandamano ya Waisrael wafuasi wa mrengo mkali wa kulia.Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Kwenye mkesha wa maandamano hayo, waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliielezea siku hiyo ya majaaliwa mwaka 1967, wakati "walipoikomboa Jerusalem na kuiunganisha."

Soma pia: Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Gaza yaendelea kwa siku ya tatu

Wawili kati ya mawaziri wa baraza lake la mrengo mkali kabisa wa kulia, Itamar-Gvir na Bezalel Smotrich, wanatarajiwa kuhudhuria maandamano ya Alhamisi.

Kufuatia vita vya siku sita vya mwaka 1967, Israel ililinyakuwa eneo la Jerusalem Mashariki na mji wake mkongwe, katika hatua ambayo haijawahi kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Netanyahu alisema "pia tunafanya hili kutokana na vitisho vinavyotuzunguka," siku kadhaa baada ya mapatano yaliyokomesha mapigano ya kuvuka mipaka na kundi la wapiganaji la Islamic Jihad la ukanda wa Gaza.

Watu 33 wakiwemo raia kadhaa waliuawa katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa, na wawili ndani ya Israel, mmoja raia na mwingine kibarua kutoka Gaza.

Kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza lilisema kabla ya maandamano ya leo kwamba linalaani kampeni ya "ukaliaji wa Israel dhidi ya watu wetu wa Palestina katika mji unaokaliwa wa Jerusalem."

Israel Palestinians Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa israel Benjamin Netanyahu anaongoza serikali ya mrengo mkali zaidi wa kulia katika historia ya Israel.Picha: Ohad Zwigenberg/AP/picture alliance

Matamshi ya ubaguzi dhidi ya Waarabu

Wakati maafisa wa Israel wanayataja maandamano hayo kama maandamano ya siku kuu, mara kadhaa yamegubikwa na matamshi ya ubaguzi dhidi ya Waarabu na vurugu dhidi ya Wapalestina wenyeji na baadhi ya waandamanaji.

Soma pia: Watu 25 wauawa katika mapigano ya Israel na wapiganaji wa Gaza

Miaka miwili iliyopita yalisababisha vita vya siku 11 kati ya Israel na wapiganaji wa Kipalestina mjini Gaza, na kundi la Hamas limewahimiza Wapalestina kuyakabili maandamano hayo mwaka huu.

Supretendant Mkuu Yoram Segal, afisa mwandamizi wa polisi mjini Jerusalem, aliwaambia maripota siku ya Jumatano kwamba safari hii wamedhamiria kuzuwia vurugu kutokea.

Segal alisema polisi imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa kijamii wa Kiyahudi na Kipalestina ili kutunza amani. Alithibitisha pia kuwa kumekuwepo na watu kadhaa waliokamatwa wakiaminika kupanga vurugu, lakini alikataa kufafanua.

Polisi wa Israel wawashambulia tena Wapalestina

Katika mtihani kuelekea maandamano hayo, karibu Wayahudi 900 walikuwa wanazuru eneo takatifu na nyeti la Jerusalem mapema Alhamisi, kwa mujibu wa Bayadenu, ambalo ni kundi la wanaharakati linalokuza ziara za Kiyahudi katika eneo hilo.

Polisi walionekana wakisindikiza makundi ya wageni wa Kiyahudi wakitembea katika eneo hilo na wabunge kadhaa wa serikali ya muungano pia waliwasili katika eneo hilo.

Soma pia: Umoja wa Mataifa walaani mauwaji ya raia Gaza

Eneo hilo la kilimani linafahamika kwa Wayahudi kama Hekalu la Mlimani, ambalo ni mahali yalipokuwa mahekalu ya kale ya Kiyahudi, na ndiyo eneo takatifu zaidi katika imani ya Kiyahudi.

Wapalestina wanalichukulia pia kama eneo takatifu, na hii leo ndiyo nyumbani kwa Msikiti wa Al-Aqsa, ambao ndiyo eneo la tatu kwa utakatifu katika dini ya Uislamu.

Chanzo: Mashirika