1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali si shwari Poland

Lilian Mtono
4 Julai 2018

Waandamanaji wanaoipinga serikali wamekusanyika mbele ya mahakama ya juu mjini Warsaw kuunga mkono utawala wa sheria pamoja na rais wa mahakama hiyo anayelazimishwa kustaafu chini ya mageuzi mapya ya sheria ya mahakama. 

https://p.dw.com/p/30muM
Polen Malgorzata Gersdorf Präsidentin des Verfassungsgerichts in Waschau
Picha: Imago/ZUMA Press/M. Wlodarczyk

Takriban waandamanaji 5,000 walikusanyika mbele ya jengo la mahakama hiyo ya juu jana usiku kama ishara ya kuwaunga mkono majaji wa mahakama hiyo, katika wakati ambapo sheria mpya ya serikali inayobatilisha umri wao wa kustaafu ikiwa tayari kuanza kutekelezwa.

Mabadiliko hayo yaliyoanza kutekelezwa rasmi saa sita za usiku, inapunguza umri wa majaji wa mahakama ya juu kutoka miaka 70 hadi 65. Aidha, inaruhusu jaji yoyote anayeguswa na sheria hiyo kuomba kibali kwa rais cha kuongezewa muda, ombi ambalo rais anaweza kulikubali ama kukataa bila ya kutoa sababu yoyote.

Majaji 27 kati ya 76 wa mahakama hiyo wanaaathirika na mageuzi hayo mapya ya sheria ya mahakama. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Poland, majaji 16 wamekwishatuma maombi.

Pawel Mucha ni msaidizi wa rais wa Poland Andrzej Duda, na alipozungumza na waandishi wa habari hapo jana alisema, majaji hao wanatakiwa kuomba kibali cha kuongezewa muda, na wasipofanya hivyo hadi leo Jumatano watakuwa wamepoteza hadhi ya kuwa majaji.

Polen | Proteste gegen Zwangsruhestand für Richter
Waandamanaji wanasema mageuzi hayo yanaligawa taifa, na huenda yakasababisha kukosekana kwa uchaguzi huru.Picha: Reuters/Agencja Gazeta/D. Zuchowicz

Jaji mkuu Profesa Malgorzata Gersdorf amekosoa vikali mageuzi hayo. Gersdorf mwenye miaka 66, aliliambia shirika la habari la DW kwamba hana nia ya kuachia nafasi hiyo kabla ya kumalizika kwa awamu yake inayotambulika kikatiba. Amesema, mabadiliko hayo hayatekelezeki, huku wakosoaji wakisema kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kudhibiti mamlaka ya mfumo wa mahakama.  

Mapema asubuhi ya leo jaji Gersdorf ameonekana akiingia kwenye jengo la mahakama hiyo, hatua inayoashiria kwamba anapingana na sheria hiyo mpya. Mara baada ya kuingia mahakamani hapo, alizungumza na wafuasi wake waliomzunguka pamoja na wapinzani wa kisiasa, akisema uwepo wake mahakamani hapo hauhusiani na siasa, bali zaidi unalenga kulinda utawala wa sheria.

Msaidizi huyo wa rais Duda alisema kwamba jaji Gersdorf atatakiwa kustaafu kulingana na sheria hiyo mpya, na mamlaka yake sasa yatachukuliwa na jaji Jozef Iwulski, aliyeteuliwa na rais Duda.

Umoja wa Ulaya ulianzisha hatua ya kisheria siku ya Jumatatu, ambayo ni ya hivi karibuni katika mvutano mkali juu ya mageuzi hayo ya mfumo wa mahakama. Kulingana na shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International, majaji wa Poland wanapitia shinikizo la kisiasa, linalofungamanishwa na mabadiliko hayo.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu wa Poland, Mateuzs Morawiecki ameliambia bunge la Ulaya hii leo kwamba mataifa wanachama yana haki ya kutengeza mfumo wa sheria katika idara zao za mahakama kwa kuzingatia tamaduni zao.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE/AFPE/DW

Mhariri: Caro Robi