1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali si shwari mjini Bangui

30 Septemba 2015

Amri ya kutotembea usiku imetolewa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa nchi hiyo inaweza kukabiliwa na ghasia mithili ya zile zilizoshuhudiwa mwaka 2013 na 2014.

https://p.dw.com/p/1GfuH
Maandamano yenye ghasia katika mitaa ya Bangui
Maandamano yenye ghasia katika mitaa ya BanguiPicha: picture-alliance/AA/H.C. Serefio

Mapigano makali yameripotiwa katika mji wa Bangui baina ya wanamgambo na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani. Makabiliano hayo yametokea pale wanajeshi hao walipokuwa wakijaribu kuondoa vizuizi katika barabara inayounganisha mji huo mkuu na uwanja wa ndege, wakati rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba Panza akirejea kutoka mjini New York alikohudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Watu 36 wameuawa katika ghasia ambazo zimeendelea kwa siku tatu katika mji huo, na wengine karibu 30,000 wamelazimika kuyahama makazi yao, kunusuru maisha. Kutokana na hofu ya mmiminiko wa wakimbizi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ni jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa upande wa Kusini, ilitangaza mara moja kuufunga mpaka wake.

Wengi wa wanaokimbia wanatafuta hifadhi karibu ya uwanja wa ndege ziliko kambi za wanajeshi wa Ufaransa na wa Umoja wa Mataifa. Mashahidi wamesema kuwa helikopta za ujumbe wa kulinda amani ujulikanao kama Sangaris zilizunguka katika anga ya uwanja wa ndege, zikiwafyatulia risasi wanamgambo.

Walinda amani watupiwa lawama

Wakazi wa Bangui wanaozikimbia ghasia hizo wamelalamikia ugumu wa kufika katika uwanja huo, wakiwashutumu wanajeshi wa kulinda amani kutotimiza majukumu yao ipasavyo, kama anavyosema mmoja wao, Erick Wilibiro. ''Tunadhani wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliotumwa huku, pamoja na Ujumbe wa Sangaris hawafanyi chochote kulinda raia. Matokeo ni yale yale kwa sababu watu wametelekezwa tena. Kusema kweli watu wamekata tamaa na hawana imani tena na wanajeshi hao''. Amesema Wilibiro.

Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameshutumiwa kutowajibika ipasavyo
Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameshutumiwa kutowajibika ipasavyoPicha: I. Sanogo/AFP/Getty Images

Rais Catherine Samba Panza alirudi nyumbani haraka kutoka mjini New York, na kabla ya kuanza safari yake alisema vurugu zimechochewa na wafuasi wa rais wa zamani wa nchi hiyo Francois Bozize. ''Tunajua kwamba vigogo wa zamani nchini humu wananuia kurudi madarakani,'' alisema rais Samba Panza.

Seleka, Anti-Balaka wajikusanya

Wakazi wa Bangui wamesema wanamgambo wa kundi la Anti Balaka, ambao ni wakristo na mahasimu wao wa Seleka ambao wao ni waislamu, walianza kujikusanya katika mji huo Jumatatu wiki hii.

Wakati huo huo ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, umekanusha ripoti kwamba wanajeshi wake waliwauwa watu watatu na kuwajeruhi wengine, wakati walipokabiliana na kundi la mamia ya waandamanaji, ambao walikuwa wakielekea Ikulu, wakidai rais Catherine Samba Panza ajiuzulu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville amesema mjini Geneva kwamba wafungwa takribani 500 wametoroka kutoka gereza la mjini Bangui usiku, na kuzidisha hofu ya kuyumba kwa usalama katika nchi hiyo inayozongwa na mzozo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo