Hali ni tulivu kwa sasa Burundi | Matukio ya Afrika | DW | 08.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hali ni tulivu kwa sasa Burundi

Mji mkuu wa Burundi, Bujumbura -kitovu cha maandamano yanayoendelea tangu siku 13 zilizopita ni tulivu kidogo hii leo katika wakati ambapo majadiliano kati ya wapinzani na wafuasi wa kiongozi huyo yanaendelea

Mwanajeshi anapita licha ya vizuwizi vya waandamanaji

Mwanajeshi anapita licha ya vizuwizi vya waandamanaji

Katika mitaa ya mji mkuu Bujumbura kitovu cha malalamiko yaliyoanza tangu April 26 iliyopita,siku moja tu baada ya Pierre Nkurunziza kuteuliwa na chama chame kugombea mhula wa tatu wa rais,hakuna tukio lolote lililoripotiwa leo asubuhi.

Katika mitaa ya Cibitoke na Nyakabiga,ripota wa shirika la habari la Ufaransa anasema amewaona baadhi ya vijana tu wakiandamana majiani,bila ya kujali mvua kubwa inayaonyesha na kiwingu kilichotanda angani.

Wakati huo huo majadiliano yaliyoanza hivi karibuni kutokana na shinikizo la jumuia ya kimataifa,kati ya wawakilishi wa serikalai na wapinzani wa mhula wa tatu wakishiriki wawakilishi wengi wa upande wa upinzani na mashirika ya jamii,yanasemekana yanaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa duru zilizo karibu na majadiliano hayo,makubaliano hayako mbali kufikiwa.Miongoni mwa duru hizo kuna wanaozungumzia uwezekano wa kuakhirishwa tarehe ya uchaguzi.Duru nyengine zinasema suluhisho la mzozo huenda likapatikana viongozi wa jumuia ya nchi za Afrika Mashariki watakapokutana Daresalam Tanzania jumatano ijayo.Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa pia limepangiwa kukutana kuzungumzia hali namna ilivyo nchini Burundi.

Hal hairuhusu uchaguzi kuitishwa kama ilivyopangwa

Nkosazana Dlamini-Zuma

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika,Nkosazana Dlamini Zuma

Umoja wa Afrika ulisema hapo awali hali si muwafak kuitisha uchaguzi wa bunge kama ilivyopangwa may 26 mwaka huu na ule wa rais mwezi mmoja baadae.Katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma alisema tunanukuu "huwezi kwenda katika nchi na kukutana na watu wanaoyapa kisogo maskani yao na kuwaambia"Tunakuja kusimamia uchaguzi.Katika hali hii ya sasa sioni vipi uchaguzi huo utafanyika"Mwisho wa kumnukuu.

Maandamano dhidi ya mhula wa tatu yameshaangamiza maisha ya watu wasiopungua 18-17 kati yao katika mji mkuu Bujumbura.Wengine wasiopungua 216 wamejeruhiwa na zaidi ya 30 elfu kuyapa kisogo maskani yao.

Nae naibu rais wa korti ya katiba aliyekimbilia uhamishoni nchini Rwanda Sylvere Nimpagaritse amesema majaji wa korti ya katiba wamelazimishwa kuidhinisha azma ya rais Nkurunziza ya kugombea mhula wa tatu.Amesema majaji walipkutana April 30 iliyopita waligundua rais Nkurunziza hana haki ya kugombea mhula wa tatu,lakini baadae majaji walianza kupokea barua za vitisho na ndio sababu ya yeye kuikimbia nchi yake.

Rais Nkurunziza apanga kutuma maombi ya kugombea wadhifa wa rais baadae hii leo

Pierre Nkurunziza, Präsident von Burundi

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Serikali ya Burundi haikusema chochote bado kuhusu madai hayo.Badala yake rais Nkurunziza anatarajiwa kutuma maombi ya kugombea mhula wa tatu mbele ya tume ya taifa ya uchaguzi baadae hii leo.Kesho ndio siku ya mwisho ya kutumwa maombi hayo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu