1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MIkururo wanazihama nyumba zao

29 Septemba 2015

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika Kati,bibi Catherine Samba Panda amefupisha ziara yake ya Umoja wa Mataifa na kutoa wito wa utulivu katika mji mkuu Bangui unaokabwa na matumzi ya nguvu tangu jumamosi iliyopita.

https://p.dw.com/p/1GfZl
Maandamano na matumizi ya nguvu mjini BanguiPicha: picture-alliance/AA/H.C. Serefio

Rais Catherine Samba Panza ametoa wito huo kupitia radio ya taifa leo hii,akiwasihi wananchi wauitike.

Kwa mujibu wa duru za karibu na ikulu ya rais,bibi Samba Panza aliyekuwa akihudhuria mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New York alikuwa akitarajiwa kurejea nyumbani leo jioni.

Kwa siku ya tatu mfululizo mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika Kati umepooza leo hii,huku waandamanaji wakiweka vizuwizi na kudai rais Samba Panza ajiuzulu.

Milio ya hapa na pale ya risasi ilisikika usiku wa jana kuamkia leo mpaka baada ya saa 12 za alfajiri-ulipomalizika muda wa sheria ya kutotoka ovyo.

Kwa mujibu wa duru za kijeshi,risasi hizo zimefyetuliwa na vikosi vya usalama vilivyokuwa vikijaribu kuwatimuwa wapora mali waliovunja vituo vya mashirika kadhaa ya huduma za kiutu.

Zaidi ya watu 36 wameuliwa na 27000 kusahama maskani yao

Kwa mujibu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa inayowahudumia wakimbizi UNHCR,matumizi ya nguvu yameshaangamiza maisha ya watu zaidi ya 36 na wengine 27 elfu kulazimika kuyapa kisogo maskani yao.

Zentralafrikanische Republik Bangui Minusca UN-Truppen
Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa MinuscaPicha: picture-alliance/AA

Wakaazi wengi wamejifungia majumbani mwao mjini Bangui wakihofia kuzuka upya matumizi ya nguvu au kuhujumiwa na wapora mali.Maelfu wengine miongoni mwa wakaazi wa Bangui wamekimbilia katika kambi za wakimbizi na hasa karibu na uwanja wa ndege kunakokutikana vituo vya vikosi vya kimataifa.

Vituo vya shirika la misaada ya dharura nalo pia limeporwa sawa na jengo la mpango wa chakula wa kimataifa PAM-kwa mujibu wa askari wa Gendarmerie wanaosema wamewatimua waporaji katika vituo kadhaa vya mashirika ya misaada ya kiutu.

Mpaka wa Jamhuri ya KIdemokrasai ya Kongo wafungwa

Wakati huo huo Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imeamua kuufunga mpaka wake na Jamhuri ya Afrika Kati kutokana na kile msemaji wa serikali ya Kinshasa anachokitaja kuwa "matumizi ya nguvu yasiyodhibitika."

Infografik Flüchtlingsströme in der Zentralafrikanischen Republik Deutsch
Picha ya jinsi wakimbizi walivyoenea Jamhuri ya Afrika Kati

"Mpaka unafungwa mpaka amri mpya itakapotolewa,kwasababu hali haidhibitiki na tunataka kuwalinda wakaazi wetu dhidi ya vurugu" amesema Lambert Mende.Kwa mujibu wa halmashauri kuu ya Umoja wa Mataifa inayowahudumia wakimbizi hadi jana mchana watu 40 wamevuka mpaka na kuingia Zongo,mji wa ncha ya kaskazini magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri Mohammed Abdul-Rahman