Hali nchini Nigeria | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 22.01.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Hali nchini Nigeria

Wanajeshi wa Nigeria wanaimarisha jitihada za kushika doria katika mji wa Jos uliokumbwa na mashambulio yaliyochochewa na uhasama wa kidini.

default

Rais wa zamani Oluseguni Obasanjo, ataka Rais Umaru Yar'adua ajiuzulu

Raia mia tatu walifariki na viongozi wa kidini wanaendelea kupanga mazishi ya pamoja. Na kama Peter Moss anavyotuarifu, kuna hali ya utulivu, na sasa serikali imepunguza muda wa amri ya watu kutotoka nje.

Mji wa Jos kwa mara nyingine tangu mwaka wa 2001 ulizongwa na masaibu ya maafa kutokana na vita na mashambulio kati ya waumini wa Kikristu na wafuasi wa dini ya Kiislamu.

Makamu wa rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, ambaye amepewa mamlaka na mahakama ya nchi hiyo kutekeleza majukumu yanayotwikwa kwa rais, ambaye anaugua nchini Saudi arabia, alikuwa ametoa amri ya raia kutotoka nje katika mji wa Jos na viunga vyake.

Hali ya utulivu imeanza kurejea na wanajeshi ,kwa ushirikano na maafisa wa polisi, wanaendelea kushika doria, wengi wao wakitembea katika vichochoro vya mji wa Jos na wengine wakizunguka mitaani wakiwa ndani ya vifaru.

Malori yaliyobeba maiti yalisindikizwa na wanajeshi kuelekea katika mazishi ya pamoja kama iliyofanyika katika uwanja wa mita 120 mraba kwenye makaburi ya Narukuta.

Wengi wa waliofariki walikuwa na alama za kupigwa visu na vidonda vya risasi kutokana na mashambulio ya magenge ya Wakristu na yale ya Waislamu.

Viongozi wa kidini wamekuja pamoja kutoa wasia kwa raia wa Jos kuishi pamoja kwa amani. Mmoja wa viongozi katika mji ulioathirika wa Jos anakiri kwamba kuna utulivu na shughuli za kawaida zitaanza kurejea

Viongozi katika eneo la Jos wameapa kutafuta suluhisho la kudumu kutatua mzozo wa kipande cha ardhi kinachozozaniwa kati ya Waislamu na Wakristu na ambacho kimepangwa kutumiwa kwa ujenzi wa makaazi ya watu walioathirika na mashambulio ya kidini mwaka wa 2008.

Kulingana na shirika la msalaba mwekundu, zaidi ya raia 17,000 wameachwa bila makao na wanahitaji msaada wa dharura.

Dawud Ahmed; ambaye ni mfanya kazi wa shirika la msalaba mwekundu nchini Nigeria, anailaumu serikali kwa kutowajibika kuwafungulia mashtaka washukiwa wa ghasia kama iliyotokea kuanzia jumapili wiki iliyopita.

Makamu wa rais Goodluck Jonathan, katika hotuba yake ya kwanza tangu aanze kutekeleza majukumu kwa niaba ya rais, alisema serikali itahakikisha wale waliohusika watafunguliwa mashtaka na hatimaye kufungwa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa; Ban Ki Moon, amesema mashambulio yaliyotokea mjini Jos yanasikitisha, naye rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, anadai rais Umaru Yar'Adua anafaa kujiuzulu kumpa nafasi makamu wake kudhibiti nchi hii yenye zaidi ya raia milioni 150.

Mwandishi, Peter Moss/Reuters

Mhariri, Othman Miraji

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com