1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Libnan na uchaguzi wa Bavaria magazetini

22 Oktoba 2012

Kitisho cha mzozo wa Syria kutapakaa hadi Libnan,uchaguzi katika jimbo la Bavaria na hali ya umaskini miongoni mwa watoto wadogo nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizohanikiza magazetini .

https://p.dw.com/p/16ULT
Machafuko mjini BeirutPicha: Reuters

Tuanzie Mashariki ya kati na machafuko ya mjini Beirut.Gazeti la "Neue Osnabrücker " linaandika:

Kwa zaidi ya mwongo mmoja Damascus ilikuwa ikishawishi mkondo wa mambo nchini Libnan.Walibnan wengi wanawachukia walowezi ambao askari kanzu wao wakikutikana kila mahala.Wengi lakini sio wote.Hadi mwaka 2005 baada ya kuuliwa waziri mkuu wa zamani,mpinzani mkubwa wa Syria,Rafik Hariri,ndipo Libnan ilipofanikiwa kuwatimuwa wanajeshi wa Syria.Kuondoka kwao kuliwawezesha walibnan waliochoshwa na vita,kujivunia hali ya utulivu kidogo.Lakini jinamizi la zamani linatishia kuzindukana.Kuna hatari yale yale ya kale,vilio na mauwaji kuanza upya:Wanamgambo,makundi ya kidini na jamii za wachache hawatachelea kuungana na kupambana hadi kufa.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linazungumzia pia wasi wasi kuuona mzozo wa Syria ukitapakaa hadi Beirut.Ggazeti linaendelea kuandika:

Balaa la Syria linavuka mpaka na kuingia Libnan kwa msaada wa gari lililoripuliwa.Hata miezi ya nyuma mapigano yalitokea katika mji wa kaskazini wa Libnan-Tripoli.Hivi sasa lakini washirika wa Assad wanaulenga mji mkuu Beirut.Sio kwamba hayo hayakutarajiwa.Rami Machluf,binaamu yake Assad alikwisha onya mwaka jana""mataifa jirani hayatakuwa tulivu ikiwa Syria haitakuwa na utulivu."Kilichoashiriwa ndicho kinachotokea.

CSU Parteitag
Kansela Angela Merkel (kushoto) na kiongozi wa chama ndugu cha CSU,Horst SeehoferPicha: dapd

Kuhusu siasa ya dani ya Ujerumani,gazeti la "Süddeutsche Zeitung" la mjini Munich linamulika uchaguzi katika jimbo la kusini la Bavaria na jinsi unavyoweza kushawishi uchaguzi mkuu ujao nchini Ujerumani.Gazeti linaendelea kuandika;

Uchaguzi wa jimbo la Bavaria unazidi kupata umuhimu siku hadi siku,watu wanapotupia jicho uchaguzi mkuu utakaofanyika pia mwakani.SPD,watakuwa na shida ikiwa makadirio yatasalia kuwa ya chini huko Bavaria na Baden Württemberg.Wakishindwa kuirekebisha hali hiyo basi mgombea wao Steinbrück atalazimika kuyazika matarajio yake:Kwa maneno mengine pindi vyama ndugu vya CDU/CSU vikishinda Bavaria,hapo kansela Angela Merkel ataondokewa na wasi wasi.

Kinderarmut in Deutschland
Umaskini miongoni mwa watoto nchini UjerumaniPicha: Getty Images

Ripoti yetu ya mwisho magazetini inahusu hali ya umaskini miongoni mwa watoto.Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha hatari ya kutumbukia katika hali ya umaskini imepungua katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Ni kweli kwamba idadi ya watoto wadogo wa familia zinazopokea malipo ya wasiokuwa na kazi kwa muda mrefu- maarufu kwa jina la Hertz-nne,imepungua.Lakini hali hiyo inatokana hasa na ukuaji wa kiuchumi na kupungua idadi ya wasiokuwa na ajira katika kipindi cha miaka iliyopita.Hakuna uhakika kwa hivyo kama watoto watafaidika kwa muda mrefu na hali hiyo.Naiwe katika maeneo ya mto Ruhr au katika miji ya mashariki ya Ujerumani:ikiwa wazee watalazimika kuishi na mishahara ya kazi ndogo ndogo za kujishikiza au malipo ya Hertz nne,basi hatari ya watoto kuuishi katika hali ya umaskini haitotoweka.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-Rahman