1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Afghanistan.

18 Agosti 2009

Hali nchini Afghanistan inawatia wasiwasi saa 48 kabla ya Wafghani kumchagua rais wao katika uchaguzi wa pili,nchini humo.

https://p.dw.com/p/JDPC
Mabango yenye picha za Rais Hamid Karzai, huko Kandahar.Picha: AP

Mripuaji wa kujitolea mhanga alijilipua karibu na kituo kimoja cha kijeshi huko Kandahar nchini Afghanistan na kuwaua watu watano, siku mbili kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo. Shambulizi lingine lilisikika katika mji wa Kabul, saa kadhaa tu baada ya roketi kuangukia makaazi rasmi ya rais Hamid Karzai.

Siku mbili tu kabla ya Wafghani kushiriki katika uchaguzi wa pili wa rais- wapiganaji wa Taliban kwa mara nyingine tena wameonya watavuruga uchaguzi wa Alhamisi- na la kutisha zaidi wamewatolea wito raia nchini Afghanistan kususia kushiriki kupiga kura.

Wahlen in Afghanistan
Maboxi ya kura, tayari kwa uchaguzi wa Alhamisi.Picha: AP

Na ilikuwa si onyo tu kutoka kwa Wataliban- misururu ya mashambulizi saa 48 kabla ya uchaguzi iliashiria walikuwa na nia ya kusambaratisha zoezi hili la kidemokrasia nchini Afghanistan. Mripuaji wa kujitolea mhanga alifuliliza moja kwa moja hadi katika kituo kimoja cha kijeshi huko Kandahar na kujiripua- matokeo wanajeshi watatu wa Kiafghani na raia wawili wakauawa. Watu wengine watano walijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Kama hili lilikuwa halitoshi, miripuko ya roketi ilisikika katika mji mkuu wa Kabul na mji wa Jalalabad, watu 10 walijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Ingawa maafisa wa utawala walithibitisha kurushwa huko kwa roketi katika mji mkuu wa Kabul, wamekuwa kimya kuhusiana na madai ya Wataliban kwamba roketi hizo zilipiga makaazi ya rais Hamid Karzai.

Vikosi vya jumuiya ya kujihami vya NATO vimesema vitasimamisha operesheni zao zote ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi. Katibu mkuu wa NATO Anders Fogh Rasmussen aliwatolea wito Wafgani wajitokeze kwa wingi ili wachukue usukani wao nchi yao- kupitia kura zao.

'' Nawaomba Wafgani wote wajitokeze kupiga kura ili wawachague viongozi wao kama ishara wanataka uhuru wa kujitawala, waonyeshe kwamba hawatafuata mkondo wa vitisho na mashambulizi kutoka kwa maadui wa Afghanistan.'' Alisema Rasmussen.

Kundi la Taliban limeonya halitaruhusu Waafgani kushiriki katika uchaguzi wa Alhamisi.

Katika taarifa fupi, Taliban walisema - '' tunawasihi raia wote walio katika emirati hii ya Kiislamu wasijaribu kushiriki katika zoezi hili la kupotosha linalongozwa na Marekani. Hivyo tunawataka watu wote wasusie uchaguzi huo.''

Flash-Galerie Wahlen Afghanistan
Mwanajeshi wa Kiafghani akishika doria.Picha: AP

Taarifa hiyo iliendelea kusema- Mujahideen wote wana jukumu kusimama imara dhidi ya maadui wa Emirati ya Kiislamu kuhakikisha mpango wao unafeli.

Jana Kundi hili la Taliban lilisambaza vijikaratasi katika vijiji va kusini- ngome ya Wataliban akionya kwamba watavamia vituo vya kupigia kura.

Wafghani milioni 17 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi wa siku ya Alhamisi kumchagua rais wao- pamoja na madiwani 420 katika mikoa au majimbo 34. Huu utakuwa uchaguzi wa pili katika historia ya Afghanistan- lakini unazungukwa na shaka shaka kufuatia hali mbaya ya usalama.

Utawala wa Taliban uliondolewa madarakani mwaka 2001- katika uvamizi uliongozwa na Marekani- na nafasi yake ikachukuliwa na serikali iliyoungwa mkono na nchi za Magharibi. Serikali ya Hamid Karzai- ambaye sasa anawania muhula wake wa pili madarakani.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri:M.Abdul-Rahman