Hali kisiwani Madagascar | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali kisiwani Madagascar

Mazungumzo ya siku tatu mjini Pretoria yameshindwa kuwatanabahisha mahasimu wa kibuki wakubali kuunda serikali ya umoja wa taifa

default

KIongozi wa Madagascar Andry Rajoelina

Kiongozi wa Madagascar, Andry Rajoelina, amesema "anaweza kuunda serikali ya mpito isiyoelemea upande wowote kisiasa", baada ya kushindwa duru mpya ya mazungumzo ya kugawana madaraka nchini Afrika Kusini. Rajoelina anasema anataraji wanajeshi wataendelea kumuunga mkono.

Baada ya miezi kadhaa ya maandamano, Andry Rajoelina alimng'oa madarakani na kwa msaada wa wanajeshi rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasi, Marc Ravalomanana, March mwaka jana .Tangu wakati huo kisiwa cha Madagascar kilioko katika bahari ya Hindi kinakabwa na mgogoro wa kisiasa.

Mwezi uliopita wanajeshi walimpa muda Rajoelina hadi April asake ufumbuzi katika wakati ambapo kiongozi huyo kijana na washirika wake mia kadhaa wanakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Afrika.

"Tumeamua-ikiwa wanasiasa wanashindwa kusikilizana, basi watu wasioelemea upande wowote watasimamia shughuli za serikali na taasisi muhimu za kisiasa", amesema Andry Rajoelina mbele ya waandishi habari.

Hakutoa maelezo zaidi, lakini uvumi umeenea kwamba serikali mpya inaweza kuundwa na wasomi, wawakilishi wa mashirika ya huduma za jamii na wanajeshi.

Mmojawapo wa washauri wake, Desiré Ramakavélo, anasema

"Yeye anaona mazungumzo pamoja na makundi mengine ndio yameshamalizika tena. Hivi sasa atalazimika kuwajibika pamoja na vikosi vya jeshi."

Andry Rajoelina hakusema bado kama anapanga kumpokonya wadhifa wake waziri mkuu ambae ni afisa wa ngazi ya juu wa kijeshi. Amesema tuu kwamba wakati wa mazungumzo umeshapita. Hata hivyo, ameongeza kusema yuko tayari kuzingatia mapendekezo ya mahasimu wake.

"Tunabidi tusonge mbele, tunalazimika kuanzisha Jamhuri ya nne-kipindi cha mpito lazima kimalizike mwaka huu." Amesisitiza Andry Rajoelina, na kusema ana hakika maoni yake yanaungwa mkono pia na wanajeshi.

Uamuzi wa mwisho unatarajiwa mnamo saa 48 zijazo.Upande wa upinzani na wakuu wa kijeshi hawajasema chochote hadi sasa.

Rajoelina, Ravalomanana na marais wa zamani, Didier Ratsiraka na Albert Zafy, walishiriki kwa muda wa siku tatu wiki iliyopita mjini Pretoria katika mkutano wa suluhu uliosimamiwa na Ufaransa, Afrika kusini na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika, SADC.

Mpatanishi wa jumuia ya SADC, rais wa zamani wa Mozambik, Joaquim Chissano, amesema mzizi wa fitina unakutikana katika suala la tarehe ya uchaguzi pamoja na msamaha kwa uhalifu uliofanyika katrika kipindi cha kabla ya kupinduliwa Marc Ravalomanana.

Rajoelina anasema atamchukulia hatua yeyote atakaejaribu kukorofisha uchaguzi utakaoitishwa kisiwani humo. Lakini wafadhili wa kigeni wameshaonya uchaguzi utakaoandaliwa na upande mmoja hautaweza kutambuliwa kama ni halali.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir/Reuters,afp

Imepitiwa na: Miraji Othman

 • Tarehe 04.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NDzl
 • Tarehe 04.05.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NDzl

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com