1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni tete nchini Sudan

Amina Mjahid
12 Aprili 2019

Utawala mpya wa kijeshi Sudan umesema utaanzisha majadiliano ya wazi na makundi yote ya kisiasa katika harakati za kuunda serikali ya kiraia, huku waandamanaji wakiendelea kumiminika mitaani kupinga utawala wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/3GhdO
Sudan Verteidigungsminister Videostill   Awad Mohamed Ahmed Ibn Auf
Picha: Reuters TV

Baraza la kijeshi limesema halitavumilia uvunjifu wowote wa amani, baada ya waandamanaji kukaidi amri ya kutotoka nje usiku na badala yake kulitaka jeshi kurejesha mara moja utawala wa kiraia.

Viongozi wa maandamano hayo wamelitaja baraza la kijeshi lililochukuwa madaraka kuanzia jana kuwa na sura zile zile za watu kutoka katika utawala uliopita, ulioitumbukiza nchi katika migogoro chungu nzima, umasikini na kutokuwa na usawa wa kijamii.

Sudan Militär und Demonstranten in Khartoum
Jeshi likishika doria huku waandamanaji wakiendelea na maandamano yao mjini Khartoum Picha: Getty Images/AFP

Wamesema tangazo la hapo jana kwamba jeshi litasimamia kipindi cha mpito nchini humo linamaanisha hakuna chochote walichokipata kufuatia maandamano yao ya muda mrefu.

"Tutaendelea na mapinduzi yetu. Tunataka utawala mzima kuondoka madarakani sio tu Bashir peke yake," alisema Ahmed mmoja ya waandamanaji. Hata hivyo, wachambuzi wanasema kupinduliwa kwa Bashir kumeifanya hatua ya kufikia demokrasia nchini Sudan kuonekana kuwa mbali zaidi.

Omar al Bashir hatopelekwa ICC anakotakiwa kwa makosa ya uhalifu wa kivita 

Utawala wa kijeshi kwa upande wake umesema una nia ya kurejesha utawala wa kiraia na hilo litafanyika kwa kuzingatia matakwa ya waandamanaji. Mwenyekiti wa baraza la kijeshi katika kamati ya kisiasa, Luteni Jenerali Omar Zain al-Abdin, amesema hawana suluhisho la kila kitu, bali mustakabali wa nchi utatokana na matakwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ya waandamanaji na kwamba hawana upande wowote au kundi lolote wanaloliegemea.

Omar al-Bashir
Rais wa Sudan aliyeondolewa madarakani Omar al Bashir Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Al-Abdin amethibitisha kuwa rais Omar al Bashir aliye na miaka 75 na aliyeiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, pamoja na viongozi wengine wa juu, akiwemo makamu wa rais na washirika wa Bashir, wako chini ya ulinzi wao. Lakini hatukutoa habari zaidi ni wapi hasa walipo viongozi hao.

Omar Zain al-Abdin ameongeza kuwa hawatamfikisha Bashir katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, anakotakiwa kwa makosa ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur, ambako watu zaidi ya 300,000 waliuwawa huku watu milioni 2.7 wakipoteza makaazi yao.

Huku hayo yakiarifiwa, mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, ameutolea wito utawala mpya nchini Sudan kuhakikisha haki za binaadamu zinalindwa na kujizuwia kutumia nguvu na kuanzisha vurugu dhidi ya waandamanaji katika mji mkuu Khartoum. Katika taarifa yake, Bachelet amesema huu ni wakati muhimu na tete kwa Sudan na kuna wasiwasi mkubwa juu ya mustakabali wa taifa hilo.