1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni tete Jerusalem

Saumu Mwasimba
9 Mei 2021

Polisi ya Israel yatoa kibali kuruhusu gwaride la kupeperusha bendera ya Israel katika mji mkongwe wa Jerusalem licha hali kuwa tete katika eneo la msikiliti wa al Aqsa

https://p.dw.com/p/3tA1Q
Israel-Palästina | Neue Zusammenstößen in Jerusalem
Picha: Oded Balilty/AP Photo/picture alliance

Polisi ya Israel imetoa kibali jumapili cha kuruhusu gwaride la maandamano ya kupeperusha bendera ya Israel. Zoezi la kila mwaka la kuadhimisha siku ya Jerusalem,siku ambayo Waisrael wanapeperusha bendera kuonesha alama ya kuimiliki  miji yote inayogombaniwa katika eneo hilo.

Gwaride hilo litafanyika siku ya Jumatatu. Ni hatua inayokuja licha ya kushuhudiwa siku kadhaa za machafuko na ongezeko la mivutano baina ya nchi hiyo ya Israel na Wapalestina katika eneo takatifu ambalo ni chanzo kikubwa cha mgogoro huu.

Gwaride hilo la Waisraeli litapita mitaa ya mji mkongwe wa Jerusalem,sehemu kadhaa  za Jerusalem Mashariki eneo ambalo lilitekwa na hatimae kunyakuliwa kwa mabavu na Israel mnamo mwaka 1967 katika vita vya Mashariki ya kati baina ya nchi hiyo na Palestina. Polisi ya Israel imeidhinisha gwaride hilo kufanyika wakati yakiendelea makabiliano baina ya Polisi na Wapalestina katika mji huo mkongwe wa Jerusalem ambako ni kitovu cha mgogoro wa siku nyingi unaoamsha hisia kali katika ulimwengu wa kiislamu.

Weltspiegel 13.04.2021 | Corona | Israel Jerusalem | Tempelberg Vorbereitung Ramadan
Picha: Ammar Awad/REUTERS

Kabla ya alfajiri ya Jumapili maelfu ya waumini wa dini ya kiislamu walipambana upya kwa mara nyingine na polisi katika lango la msikiliti mtakatifu wa Al-aqsa kwenye mji huo mkongwe.  Vidio zilizorushwa kwenye majukwaa mbali mbali ya mitandao ya kijamii

ziliwaonyesha Wapalestina wakirusha chupa za maji na mawe dhidi ya maafisa wa polisi waliokuwa wakifyetua maguruneti ya mkono.

Amos Gilad, aliyewahi kuwa afisa mwandamizi wa ulinzi wa Israel akizungumza na kituo cha redio ya Jeshi amesema kwamba gwaride hilo la maadhimisho ya siku ya Jerusalem linapaswa kufutwa au kuelekezwa kupita njia nyingine kando na eneo la Lango la Damascus la mji huo mkongwe wa Jerusalem kwasababu mripuko unaweza kutokea muda wowote.

 Lakini msemaji wa polisi ya Israel Eli Levi leo Jumapili amesema kwamba hakuna mipango ya kuzifuta sherehe hizo licha ya kuwepo uwezekano wa kuzusha vurugu zaidi.

Israel Jerusalem Israelische Nationalisten Gedenken Hadassah Massaker
Picha: picture-alliance/Zuma/N. Alon

Ifahamikwe kwamba eneo la msikiti  al-Aqsa linaagaliwa kama eneo la tatu takatifu kwa waumini wa kiislamu wakati wayahudi nao wanasema ni eneo lao takatifu. Ni sehemu ambayo miaka nenda rudi limekuwa chachu ya mapigano makali na mara hii wapalestina chungunzima walijeruhiwa kwenye vurugu zilitotokea kwenye eneo hilo usiku kuanzia Jumamosi hadi Jumapili wakati Waislamu wakiadhimisha kile kinachoitwa usiku mtakatifu,au Laylat-al-adr,usiku unaoaminika kwa waislamu kwamba ndipo ilipoteremshwa Quran,kitabu kitakatifu katika mwezi wa mfungo wa Ramadhan.

 Siku ya ijumaa zaidi ya Wapalestina 200 walijeruhiwa katika vurugu zilizotokea ndani ya eneo la ua wa msikiti wa  Al-Aqsa na kusabaisha washirika mbali mbali wa Israel wa nchi za kiarabu kutowa kauli za kulaani tukio hilo  huku nchi kama Marekani,Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ukitowa mwito wa utulivu. Kwa upande mwingine waziri mkuu Benjamin Netanyahu amesema Israel inapingwa kwa nguvu zote shinikizo la kuitaka ikomeshe ujenzi wa makaazi Jerusalem.

Bildergalerie - Orte und Städte vor Kriegsbeginn
Picha: Imago/United Archives

Ni baada ya Jumuiya ya kimataifa kulaani hatua iliyopangwa ya kuwaondowa kwa nguvu wapalestina kutoka kwenye makaazi yao katika mji wanaoutaka kwa mabavu walowezi wakiyahudi.Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ametowa mwito wa vurugu kukomeshwa Jerusalem na kuzitaka pande zote kutafuta suluhisho ili kuheshimu utambulisho wa imani zote katika mji huo mtakatifu.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sudi Mnette