1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna ushahidi Kombe la Dunia 2006 lilinunuliwa

4 Machi 2016

Ripoti ya uchunguzi ulioanzishwa kuhusiana na tuhuma kuwa Ujerumani ilinunua kura za kupewa kibali cha kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2006 imesema kuwa haiwezi kufuta uwezekano kuwa hongo zilitolewa

https://p.dw.com/p/1I7Vp
Deutschland Leipzig Franz Beckenbauer (l) und FIFA-Präsident Joseph Blatter
Picha: picture-alliance/dpa/T. Eisenhuth

Christian Duve kutoka kampuni ya sheria ya Freshfields iliyopewa jukumu na Shirikisho la Kandanda Ujerumani – DFB kuchunguza madai hayo, amesema kuwa “hawana ushahidi kuwa kura zilinunuliwa, lakini hawawezi kufuta uwezekano huo”.

Duve hata hivyo ameongeza wameweza kuona kuwa huenda kulikuwa na mabadiliko katika mpangilio wa upigaji kura na hilo huenda liliwaathiri maafisa wa FIFA barani Asia.

Kutokana na badai hayo, rais wa zamani wa DFB Wolfgang Niersbach alidai kuwa shirikisho hilo liliipa FIFA faranga milioni 10 ili lipewe ruzuku ya kiasi cha faranga milioni 170. Na ripoti ya Freshfields imethibitisha kuwa DFB ilikopa fedha hizo kutoka kwa aliyekuwa mkuu wa Adidas marehemu Louis-Dreyfus , lakini imesema ilishindwa kupata uwazi kuhusu kile fedha hizo zilifanya.

Shirikisho la Kandanda la Kimataifa – FIFA limeikaribisha ripoti ya uchunguzi hio likisema litaitathmini kwa umakini na kuyajumuisha matokeo yake katika uchunguzi wake wa ndani kuhusu suala hilo.

Rais mpya wa DFB

Wakati huo huo, Shirikisho la kandanda la Ujerumani – DFB linatarajiwa kumtangaza Reinhard Grindel kuwa rais wake mpya mnamo Aprili 15.

Grindel mwenye umri wa miaka 54 atakuwa mrithi wa kudumu wa Wolfgang Niersbach ambaye alijiuzulu mwezi Novemba kutokana na tuhuma za rushwa zinalohusiana na ombi la Ujerumani la kuandaa dimba la Kombe la Dunia mwaka wa 2006.

Grindel ambaye ni mwanachama wa sasa wa bunge la Ujerumani, ni makamu wa rais wa zamani wa Shirikisho la Kandanda la jimbo la Saxony. Alikuwa mwekahazina wa DFB mwaka wa 2013 na akapendekezwa kumrithi Niersbach mwezi Novemba. Anaungwa mkono kwa kauli moja na wajumbe wa DFB na ligi ya Kandanda Ujerumani DFL na huenda akawa rais wa 12 wa shirikisho la kandanda nchini humo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu