1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna tena Love Parade

26 Julai 2010

Mwaka huu,tamasha maarufu kabisa la muziki "Love Parade" limegubikwa na msiba mkubwa.Watu 19 wamepoteza maisha yao na zaidi ya watu 340 walijeruhiwa katika mkanyagano uliotokea wakati wa tamasha hilo la midundo ya tekno.

https://p.dw.com/p/OV86
Blumen und Kerzen stehen am Sonntag, 25. Juli 2010, in Duisburg an der Stelle, wo am Samstag, 24. Juli 2010, bei der Loveparade eine Massenpanik zum Tot von 19 Teilnehmern fuehrte. (apn Photo/Hermann J. Knippertz) --- Flowers and candles are lying at the scene in Duisburg, Germany, on Sunday, July 25, 2010, where 19 persons died in a panic on yesterday's loveparade. (apn Photo/Hermann J. Knippertz)
Maua na mishumaa iliyowekwa eneo ambako watu 19 walipoteza maisha yao,wakati wa tamasha la Love Parade, Jumamosi, 24 Julai,2010.Picha: AP

Wakati mjini Duisburg na kote nchini Ujerumani, lawama zikizidi kutolewa kuhusu utaratibu wa usalama, siku ya Jumapili, kwenye mkutano wa waandishi wa habari, waandalizi wa tamasha hilo la muziki "Love Parade" walitangaza mwisho wa tamasha kubwa kabisa la midundo ya tekno.

"Ni mwisho wa Love Parade - kwa kherini"

Hivyo ndio ilivyotangazwa kuwa tamasha hilo, lililovutia watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, halitoandaliwa tena nchini Ujerumani. Mashahidi wa maafa yaliyotokea mjini Duisburg wamekubali kuwa "Love Parade" limegubikwa na msiba mkubwa na itakuwa vigumu sana kuendelea na tamasha hilo.

Kile kilichotokea tarehe 24 Julai mwaka 2010 kwenye uwanja wa stesheni ya zamani ya treni, mjini Duisburg, hakipaswi kutokea tena nchini Ujerumani. Vijana 19 kutoka Ujerumani na nchi za kigeni wamepoteza maisha yao na wengine wapo hospitali mahututi. Mashahidi wakijaribu kueleza yale yaliyotokea walisema:

"Waliparamia wenzao ili kufikia ngazi na ukuta - mradi watoke kwenye msongamano huo."

Na mwenzake akaongezea:

" Watu walikuwa wakiuparamia ukuta na wengine walidondoka kwenye umati. Ni vigumu sana kuamini, jambo kama hilo limetokea Ujerumani."

Wageni wengi wanatoa lawama kali dhidi ya waandalizi wa tamasha hilo. Wanasema utaratibu wa usalama ulikuwa na dosari.Watu walibanana katika eneo dogo na kulikuwepo uwezekano mdogo wa kukimbia msongamano. Njia kuu ya kuingilia uwanjani ni ujia wenye upana wa mita 20 unaopitia chini ya daraja kwa urefu wa kama mita 200. Umati wote ulipitia ujia huo. Watu kutoka pande mbili za barabara walikutana kwenye ujia huo ulioelekea uwanjani. Hapo ndio kulikotokea msongomano ulioishia kwa msiba mkubwa. Kwani hakuna alieweza kwenda mbele wala kurudi nyuma. Vijana wengine waliparamia ukuta na wakaporomoka kwenye umati.

Licha ya maafa hayo, tamasha hilo la muziki liliendelea hadi jioni. Waandalizi walihofia msongomano mpya, pindi tamasha hilo lingekatizwa kwa ghafula. Meya mkuu wa mji wa Duisburg, Adolf Sauerland alijaribu kuwatupia lawama vijana walioparamia vizuizi. Lakini hakuna hivi wala vile, mji wa Duisburg na waandalizi wa tamasha la Love Parade, hawana budi kuwajibika.

Mwandishi: Petersmann,Sandra/ZPR/P.Martin

Mhariri: Charo, Josephat