1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna msaada wa jumla jamala!

P.Martin - (DPA)2 Machi 2009

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels,maafikiano ya nyongeza ya mishahara katika sekta ya hudumu za jamii ni mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatatu.

https://p.dw.com/p/H3xP

Tukianza na DIE WELT gazeti hilo linaandika juu ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya. Linasema:

Kilichodhihirika ni kuwa nchi za Umoja wa Ulaya angalau zinakubaliana kuwa zinakabiliwa na mzozo mkubwa kabisa wa fedha na uchumi kwa kiwango ambacho hakijapata kushuhudiwa tangu zaidi ya nusu karne iliyopita. Vile vile mataifa hayo yanatambua kuwa hata ikiwa ni vugumu, hayana budi kupitisha maamuzi fulani ili kutoa fursa ya kuanza upya.

Likiendelea DIE WELT linasema, lakini Hungary imeonyesha vipi mtu anaweza kuipoteza fursa hiyo,kwani hata kabla ya viongozi wa serikali kuanza kujadiliania vipi kwa pamoja wataweza kukabiliana na mgogoro wa kifedha na kiuchumi katika Umoja wa Ulaya,waziri mkuu wa Hungary ametaka kuanzishwe mfuko maalum kusaidia nchi za Ulaya Mashariki ili kuzuia mtengano kati ya magharibi na mashariki,kama wakati wa vita baridi.

Lawama kama hizo hazina nafasi katika wakati huu mgumu .Kwa hivyo wala haishangazi kuwa pendekezo lake lilipingwa - hakutokuwepo mpango maalum kusaidia nchi za mashariki - msaada utatolewa kwa kuzingatia hali ya nchi moja moja na sio jumla jamala.

Gazeti la SÜDKURIER likikubaliana na uamuzi huo linaeleza hivi:

Kuna sababu nzuri za kukataa kuitikia "AMEEN" kwa kila dai linalotolewa. Kwani baadhi ya nchi zimeathirika vibaya sana na zingine kidogo.Kwa hivyo hakuna dawa moja kwa wote.

Tukibadilisha mada gazeti la RHEINISCHE POST linasema, huu si wakati wa kudai nyongeza ya mishahara.Linaongezea:

Wakati ambapo mamilioni ya wafanyakazi katika sekta binafsi za uchumi na viwanda wanahofia nafasi zao za ajira,wafanyakazi katika sekta ya huduma za jamii majimboni,wanapewa nyongeza ya asilimia 3 moja kwa moja - na asilimia 1.2 mwaka mmoja baadae.Isitoshe, waajiriwa hao wala hawana haja ya kuwa na wasiwasi kuwa waajiri wao watafilisika.

Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linasifu makubaliano yaliyopatikana kati ya waajiri na vyama vya wafanyakazi katika sekta ya huduma za jamii.

Naam,kwani kwa maoni ya gazeti hilo si jambo dogo kuwa maafikiano yamepatikana haraka hivyo wakati ambapo kila sekta inakabiliana na hali mbaya kifedha na kiuchumi.Hapo si waajiriwa tu waliofurahi kupata nyongeza ya mishahara wakati ulimwengu mzima ukikumbwa na uchumi unaodorora.

Bila shaka waajiri pia wamepumua kwani nyongeza hiyo si asilimia 8 kama ilivyodaiwa.Vile vile wana hakika kuwa kwa miezi 22 ijayo hakutokuwepo wimbi la migomo.Ikiwa wafanyakazi hao watatumia nyongeza hiyo kufufua uchumi wa Ujerumani,basi kila mmoja atanufaika kutokana na maafikiano yaliyopatikana.