1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna meli iliyo salama mbele ya maharamia wa Kisomali

P.Martin19 Novemba 2008

Miongoni mwa mada zilizogongwa vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatano ni utekaji nyara wa meli iliyopakia mafuta nje ya pwani ya Somalia.

https://p.dw.com/p/Fxx7

Ripoti mpya ya PISA-utafiti uliofanywa na tume ya OECD-kuhusu viwango vya elimu barani Ulaya imeshughulikiwa pia.Lakini tutaanza na utekaji nyara wa meli nje ya pwani ya Somalia.Gazeti la OSTSEE ZEITUNG kutoka Rostock linasema,hakuna tena meli iliyo salama mbele ya maharamia wa Kisomali.Jumuiya ya kimataifa sasa lazima ichukue hatua kukomesha balaa hiyo katika Pembe ya Afrika.Umoja wa Ulaya umetambua hilo.Kwa hivyo hadi kati kati ya mwezi wa Desemba,manowari za majeshi ya majini zitapelekwa katika enea hilo.

Lakini gazeti la MÄRKISCHE ZEITUNG kutoka Potsdam linawasi wasi na linaeleza hivi:

Ni shida kuamini kuwa nchi za magharibi zinataka kuzuia ugaidi katika Pembe ya Afrika,lakini zinashindwa kudhibiti uhalifu wa maharamia.Kwani kuambatana na sheria za hivi sasa,hali ya hatari inapozuka manowari za Ujerumani zilizopo mbele ya pwani ya Djibouti zinaruhusiwa kuchukua hatua dhidi ya maharamia.Hiyo ilisaidia kuzuia utekaji nyara wa meli kadhaa. Lakini tatizo ni kwamba meli zilizotekwa nyara zinapoomba msaada,jeshi la wanamaji haliruhusiwi kushambulia.Na hiyo ni kashfa kubwa-yaani ujambazi unatokeo mbele ya manowari yenye silaha nzito.

Mada nyingine iliyoshughulikiwa magazetini leo hii ni ripoti ya PISA kuhusu viwango vya elimu shuleni.NORDWEST-ZEITUNG kutoka Oldenburg na matokeo ya utafiti uliofanywa:

Yadhihirika kuwa pigo la miaka minane iliyopita limekuwa na athari zake nchini Ujerumani.Kwani hata mikoa iliyokuwa nyuma kabisa katika ripoti ya viwango vya elimu,imesonga mbele.Sasa mkoa wa Saschsen uliopiga fora hauna haja ya kuona aibu kulinganishwa na viwango vya kimataifa. Likiendelea linasema,matokeo hayo lakini hayaelezi cho chote kuhusu mfumo wa elimu nchini Ujerumani - si utaratibu wa kuwatenganisha wanafunzi mapema na kuwagawa katika shule zenye mifumo mitatu tofauti wala utaratibu wa kuwaweka pamoja kwa muda mrefu katika shule ya aina moja.Suluhisho pekee ni kuwa na walimu zaidi na madarasa yenye wanafunzi wachache;kuongeza idadi ya shule za siku nzima na vile vile watoto wanaotoka katika mazingira ya umasikini wapewe motisha.Kwa kufanya hivyo ndio Ujerumani labda itaweza kuwa katika kundi linaloongoza kimataifa katika ripoti ya PISA.

Gazeti la CELLESCHE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linaeleza hivi:

Mijadala juu ya sera za serikali kuhusu mfumo wa elimu,ingali ikiendelea na hakuna ishara kuwa itamalizika hivi kariibuni.Lakini moja limedhirika: Walimu zaidi na wanafunzi wachache darasani ndio kinachohitajiwa ili wanafunzi waweze kufanikiwa,na hiyo iwe katika shule za kila aina.

Mwenye chongo asimcheke mwenye kengeza linasema FLENSBURGER TAGEBLATT kuhusika na mameneja wa makampuni na benki wanaokosolewa na wanasiasa kufuatia mgogoro wa fedha. Likiendelea linaeleza hivi:

Hata wanasiasa wanapaswa kukumbuka yale yaliyosemwa na wahenga.Inajulikana kuwa kwa miaka na miaka wanasiasa walihisi wakidharauliwa na mameneja wenye kiburi.Lakini sasa mambo ndio yamegeuka.Na Waziri wa Fedha wa Ujerumani Peer Steinbrück anafurahia hali hii mpya.Yeye ametoa masharti kwa mameneja wanaomba msaada wa fedha serikalini na amewataka wawe na tahadhari zaidi pesa za watu wengine zinapohusika.Lakini gazeti hilo linauliza je serikali nayo itumie vipi fedha za walipa kodi?Ikiwa ni tamaa ya mameneja kupata faida,au sera za viongozi kujijenga,hapo walio wahanga ni raia wa kawaida lamalizia FLENSBURGER TAGEBLATT.