Haki za binaadamu mashakani Sudan Kusini - Umoja wa Mataifa | Matukio ya Afrika | DW | 02.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

SUDAN KUSINI

Haki za binaadamu mashakani Sudan Kusini - Umoja wa Mataifa

Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binaadamu nchini Sudan Kusini imeelezea wasiwasi wake juu ya kuzorota kwa hali nchini humo, huku ubakaji na ukatili dhidi ya wanawake ukiripotiwa kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi, Kenya, siku ya Ijumaa (Novemba 2), mwenyekiti wa tume hiyo, Bi. Yasmin Sooka, alielezea kusikitishwa kwake na msururu wa visa vya dhuluma za kingono zinazofanywa na makundi ya wapiganaji pamoja na wanajeshi.

"Tume hii ilipokea ripoti za wanajeshi waliowadhulumu wanawake nje ya kambi ya wakimbizi, punde tu tulipowasili Sudan Kusini. Licha ya unyanyapaa aliokuwa akikabiliana nao, mmoja wa wanawake hao alituhadithia jinsi alivyobakwa na kutishiwa kuuawa na wanajeshi", alisema Bi Sooka.

Tume hiyo ilisikiliza ripoti za wasichana na kinamama waliotekwa nyara katika kambi za wakimbizi wa ndani na kudhulumiwa kimapenzi.

Uchunguzi umebainisha kwamba katika mji mkuu wa Juba, wanawake wamekuwa wakidhulumiwa kimapenzi tangu mwezi Disemba 2013.

"Ni nambo la kusikitisha kuona kwamba kumekuwa na visa vya kikatili ambavyo yanafanywa nje ya kambi za wakimbizi, huku wanajeshi wa kulinda amani wakitazama," alisema mjumbe wa tume hiyo, Kenath Scott.

Tume hiyo yenye wanachama watatu imepewa mamlaka na Umoja wa Mataifa kuchunguza na kutoa ripoti ya hali ya haki za binadamu nchini humo na kutoa mwongozo kwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa kuhusu haki na uwajibikaji.

"Tume yetu inatoa wito kwa kufanyika uchunguzi maalum kufanywa juu ya dhuluma za kimapenzi zinazohusiana na mizozo ili kukusanya ushahidi utakaotumika kuwashtaki washukiwa siku za baadaye," alisema Bi Sooka.

Hata wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa wameripotiwa kufanya vitendo vya dhuluma kwa wanawake kwa mujibu wa tume hiyo.

Ripoti hii inakuja mwezi mmoja baada ya Kenya kuondoa wanajeshi wake baada ya kiongozi wa Kikosi cha Kulinda Amani, Luteni Jenerali Johnson Mogoa Kimani Ondieki kutoka Kenya, kuachishwa kazi na Umoja wa Mataifa.

Tume hiyo itatoa ripoti yake kwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi 2017.

Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef