1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haki ya Ukimbizi na Sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu Ukimbizi

Charo Josephat/ Hasselbach27 Machi 2009

Lampedusa na Malta ni mwisho wa safari ya wakimbizi wengi kutoka Afrika wanaotaka kuingia Ulaya

https://p.dw.com/p/HKgj
Wakimbizi haramu wakiwa katika kisiwa cha LampedusaPicha: dpa - Fotoreport

Kwa miaka mingi maelfu ya Waafrika wamekuwa wakisafiri kuja barani Ulaya kupitia njia zinazohatarisha maisha yao. Wakiwa katika boti zao mara kwa mara hutia nanga katika visiwa vya Lampedusa na Malta. Watu wengi hufa huku wakijaribu kuingia Ulaya kwa njia ya baharini. Wanaofaulu kufika kwenye visiwa hivyo vya Umoja wa Ulaya huwekwa katika kambi. Mwandishi wetu Christoph Hasselbach mjini Brussels Ubelgiji anasema Umoja wa Ulaya unajadili sera muafaka kukabiliana na wakimbizi hao kutoka Afrika. Ripoti yake inasomswa humu studioni na Josephat Charo.

Wakati kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na maswala ya sheria, Jacques Barrot, alipozitembelea kambi za Lampedusa na Malta, alionekana kukasirishwa na hali ilivyo katika kambi hizo. Akizungumza mjini Brussels Ubelgiji, msemaji wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Johannes Laitenberger, amezitaka nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zisadie kuratibu sera itakayofaa kukabiliana na wakimbizi kwenye kambi hizo.

"Sera za halmashauri katika hali hii ni kuratibu mshikamano ili tuweze kufanya tunachopaswa kukifanya kwa ajili ya wakimbizi na pia tuweze kuwasaidia walio katika hali ngumu wakijaribu kukabiliana na changamoto hii."

Mshikamano katika kuwachukua wakimbizi hao ni swala moja muhimu. Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, aliwahi kueleza mnamo mwaka 2005 vipi Umoja wa Ulaya unavyoweza kulitatua tatizo la wakimbizi. Bwana Schäüble anasisitiza kuwa mbali na kuilinda mipaka ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya inayotumiwa na wakimbizi kuingilia Ulaya, kuna haja ya nchi za umoja huo kuendelea na juhudi za kuzuia wimbi la wakimbi kuingia Ulaya na kushirikiana na nchi jirani.

Kwa msingi huu, Umoja wa Ulaya umekuwa ukijaribu tangu miaka kadhaa iliyopita kuimarisha juhudi zake kuzuia wimbi la wakimbizi kutoka barani Afrika. Hata hivyo wakosoaji wanasema sera za Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi zinakita sana katika ulinzi. Miongoni mwa wakosoaji hao ni kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya wakimbizi, Antonio Guterres, ambaye tayari mwaka 2006 alitaka kutafutwe suluhisho la kudumu la tatizo la wakimbizi barani Ulaya.

"Ulinzi bora na uwezo zaidi wa kufikia suluhisho la kudumu katika maeneo wanakotokea wakimbizi, ni lengo linalostahili kufuatiliwa. Lakini hili haliwezi kufanywa kwa kupuuza jukumu la Ulaya kutoa ukimbizi kwa wale wanaouhitaji. Ulaya ni bara la uhamiaji na lazima libakie kuwa bara la uhamiaji."

Mbunge wa chama cha Social Democratic, SPD, hapa Ujerumani, Wolfgang Kressl-Dörfler, miaka minne iliyopita aliitembelea kambi ya Lampedusa pamoja na kundi la wabunge wengine. Alishtushwa sana na hali aliyoiona kwenye kambi hiyo ya wakimbizi. Kufikia sasa mwanasiasa huyo anasema haoni ufanisi wowote uliopatikana tangu wakati huo. Maafisa wanaosimamia kambi hiyo wanajaribu kutumia mamlaka yao kuwaorodhesha wakimbizi wote kuwa wasio halali.

Aidha bwana Wolfgang Kressl-Dörfler amesema wakimbizi hawaelezwi kuhusu haki zao za ukimbizi badala yake hukamatwa na kurudishwa nchini kwao. Amesema halmashauri ya Umoja wa Ulaya haifanyi mengi kuzikumbusha nchi kama vile Italia kuhusu majukumu yao kwa wakimbizi. Inaonekana wazi dhahiri shahiri kwamba Umoja wa Ulaya hauna mshikamano katika swala hili la wakimbizi na hivyo basi itachukua muda mrefu kabla kuunda sera ya pamoja kuhusu tatizo la wakimbizi.

Mwandishi:Hasselbach/Charo

Mhariri: Abdul-Rahman