1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo
default

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 28.11.2021 | 14:00

Israel yaonesha mashaka ya Iran kuondolewa vikwazo

Israel imeonesha wasiwasi mkubwa wa huenda mataifa makubwa yataiondolea Iran vikwazo kwa makubaliano yasiyo ya kuridhisha katika kuachana na mpango wake wa nyuklia.Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa taifa hilo, Naftali Bennet, ikiwa kabla ya kuanza kwa mazungumzo mapya ya mzozo wa nishati ya Iran na mataifa makubwa kwa zingatio la makubaliano ya 2015.Waziri Mkuu Bennett aliliambia baraza lake la mawaziri kupitia televisheni kwamba ujumbe huo wanauwasilisha kwa yeyote iwe kwa Marekani au kwa taifa lingine lolote linalofanya mazungumzo na Iran.Kauli hiyo inatolewa wakati ambapo Mwanadiplomasia wa Iran, Mohammadreza Ghebi, akinukuliwa na shirika la habari la Iran, ISNA, kwamba timu ya Iran iliwasili mjini Vienna jana Jumamosi na kuanza mikutano katika ngazi ya wataalamu ambayo inahusisha viongozi wa timu za majadiliano za Urusi na China pamoja na mratibu wa Umoja wa Ulaya, Enrique Mora.

NATO yasema mgogoro wa mpakani mwa Belarus haujamalizika

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami (NATO), Jens Stoltenberg, ameonya kuwa mzozo wa wahamiaji katika mpaka wa mashariki mwa Umoja wa Ulaya bado haujakwisha, katika wakati ambapo wakimbizi kutokea Belarus wanajaribu kuingia katika eneo hilo kinyume cha sheria.Akizungumza na kituo cha televisheni cha Latvia, Stoltenberg amesema mzozo huo umepungua makali tofauti na ilivyokuwa hapo awali lakini ni mapema mno kusema umemalizika.Mvutano umeongezeka kwa majuma kadhaa sasa, baada ya wahamiaji kutoka Iraq, Yemen, Syria, Afghanistan au Iran kutaka kuvuuka na kuingia katika eneo la Umoja wa Ulaya ambapo mataifa ya Poland, Lithuania na Latvia yameathiriwa vibaya.Wengi wanaamini mzozo huo umetengenezwa kwa makusudi na mtawala wa muda mrefu wa Belarus, Alexander Lukashenko, katika kile kinachoelezwa kuwa analipiza kisasi dhidi ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa serikali yake.

Jeshi la Ujerumani kuwasafirisha wagonjwa wa Covid-19 kutoka jimbo la Bavaria kwenda Hamburg

Jeshi la anga la Ujerumani lipo katika maandalizi ya kuwasafirisha wagonjwa wa Covid-19 kutoka katika eneo lenye maambukizo mengi huko jimboni Bavaria na kwenda kupatiwa huduma za matibu mjini Hamburg.Hatua hiyo ina lengo la kupunguza msongamano mkubwa wa wagonjwa katika vyumba vya matibabu kwenye maeneo ambayo yameathiriwa zaidi na wimbi la nne la maambukizo ya virusi vya corona.Ndege ya kuwasafirisha wagonjwa chapa A310 MedEvac ndiyo itakayowachukuwa wagonjwa kutoka Munich hadi katika jiji la kaskazini la Ujerumani, katika kipindi hiki ambacho hospitali zikielezwa kuzidiwa kutokana na kasi ya ongezeko ya maambukizo katika jimbo la Bavaria.Ndege hiyo yenye uwezo wa kuwasafrisha wagonjwa sita mahututi kwa wakati mmoja imekwisha wasili mjini Munich, ikitokea mjini Cologne eneo ambalo kwa kawaida ndio maskani yake.

Uingereza yataka kuitisha mkutano wa dharura na Ulaya baada ya kutengwa na Ufaransa

Serikali ya Uingereza leo hii imetangaza mipango ya kufanya mazungumzo yake yenyewe juma hili na mawaziri wa Ulaya kuhusu mzozo wa wahamiaji baada ya kuzuiwa kushiriki katika mkutano wa mzozo wa Ufaransa.Waziri wa Mambo ya Ndani wa taifa hilo, Priti Patel, alizuiwa kushiriki mkutano wa Jumapili wa Calais, baada ya Waziri Mkuu Boris Johnson kusambaza ujumbe wa barua kwa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa akielezea matakwa ya serikali yake yanayopaswa kuchukuliwa hatua za pamoja.Kufuatia tukio la kuzama na kufa maji kwa watu 27 kwenye mlango bahari wa kuingia Uingereza Jumatano iliyopita, Patel ameandika kupitia Twitter kwamba ataitisha mkutano wa dharura na wenzake wa Ulaya kwa lengo la kudhibiti maafa zaidi katika eneo hilo. Hata hivyo, hakujawa na maelezo zaidi kuhusu eneo au hata muda wa mazungumzo.Lakini leo hii mawaziri kutoka mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Ubelgiji wanakutana katika mji wa bandari wa kaskazini ya Ufaransa wa Calais kufuatia vifo hivyo 27 vya raia wa jamii ya Kikurdi ya Iraq, tukio ambalo linalezwa kutokea wakati wakivuka kutoka Ufaransa kwenda Uingereza wakiwa katika boti dhaifu.

Burhani awafuta kazi maafisa waandamizi wa usalama wa taifa

Kiongozi mkuu wa jeshi wa Sudan, Jenarali Abdel Fattah al-Burhan, amewafuta kazi majerali wanane, ambao ni maafisa wa intelijensia na kumbadilisha mkuu wa usalama wa taifa. Habari hiyo ni kwa mujibu wa shirika la habari Reuters ambalo limevinukuu vyanzo viwili tofauti.Taarifa hii inafuatia kuteuliwa kwa mkuu mpya wa usalama wa taifa, ikiwa ni wiki moja baada ya jeshi kufikia makubaliano ya kumrejesha katika wadhifa wake Waziri Mkuu Abdallah Hamdok, ambaye aliwekwa katika kizuizi cha nyumbani, baada ya mapinduzi ya Oktoba 25.

Papa atoa wito wa kuwasaidia wahamiaji

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis amezitolea wito serikali duniani kote kuongoza jitihada katika kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi, huku akitangaza kusitisha ibada kutokana na kasi ya ongezeko la maambukizo ya virusi vya corona.Kauli hiyo ya Papa Francis katika kanisa kuu la Mtakatifu Petro ilionekana kuzilenga serikali na majeshi, huku akielezea kuhuzunishwa na vifo vilivyotokea katika eneo la mlango bahari wa kuingia Uingereza, mpaka wa Poland na Belarus pamoja na Bahari ya Mediterania.Papa Francis ana mpango wa kwenda Cyprus na baadaye Ugiriki, katika ziara ambayo imepangwa kuanza Alhamis, ambapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kukutana na wakimbizi.

Waziri mkuu wa zamani wa Cambodia afariki dunia

Waziri Mkuu wa zamani wa Cambodia, Mwanamfalme Norodom Ranariddh, amefariki dunia nchini Ufaransa. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa waziri wa habari wa Cambodia, ambaye ameisambaza kupitia ukurasa wa Facebook.Chama cha siasa cha Mwanamfalme Ranariddh aliyekuwa na umri wa miaka 77 kilishinda uchaguzi wa mwaka 1993, na aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi ya 1997.Mapinduzi hayo yalifanywa na mshirika wake wa muungano na hasimu wa kisiasa, Hun Sen, ambaye alisalia madarakani kama waziri mkuu wa Cambodia kwa zaidi ya miaka 20.

Sikiliza sauti 09:48