Guy Scott ndiye Kaimu rais wa Zambia | Matukio ya Afrika | DW | 29.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Guy Scott ndiye Kaimu rais wa Zambia

Serikali ya Zambia imemchagua makamu wa rais Guy Scott, mzambia mwenye asili ya kizungu kuwa kaimu rais wa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika hadi pale uchaguzi utakapofanyika ndani ya siku 90.

Kaimu rais wa Zambia Guy Scott

Kaimu rais wa Zambia Guy Scott

Scott amekuwa kaimu rais hii leo baada ya kifo cha rais Michael Sata kilichotokea mjini London Jumanne Jioni. Guy Scott sasa ni kiongozi wa kwanza mzungu katika taifa la kiafrika tangu F.W. de Klerk, rais wa mwisho katika enzi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini iliomalizika mwaka wa 1994.

Rais Michael Sata aliye na miaka 77 aliondoka Zambia kuelekea jijini London zaidi ya wiki moja iliopita kwa matibabu ya ugonjwa ambao bado mpaka sasa haujawekwa wazi. Sata aliandamana na mke wake pamoja na watu wengine wa karibu wa familia yake. Kwa mujibu wa katibu Msiska, Rais Sata alifariki Jumanne jioni.

Rais wa Zambia Michael Sata

Rais wa Zambia Michael Sata

Lakini vyombo vya habari awali vilikuwa vimeripoti Sata aliruhusiwa kutoka hospitali ili apate matibabu chumbani mwake huko nchini Uingereza. Rais huyo wa Zambia ameiongoza nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, ya pili kwa ukubwa wa uzalishaji shaba tangu mwaka wa 2011.

Katibu wa bunge la Zambia Rowland Msiska ametoa wito wa kuwepo utulivu nchini humo huku akisema taarifa ya mipango ya mazishi itatolewa hivi karibuni. Wasiwasi wa hali ya afya ya Sata ulianza pale rais huyo aliposhindwa kuonekana hadharani kuanzia mwezi wa Juni mwaka huu.

Wiki iliopita Waziri wa Ulinzi Edgar Lungu aliongoza sherehe za kuadhimisha miaka 50 tangu nchi hiyo ilipojipatia Uhuru wake kutoka kwa Uingereza.

Hali ya afya ya rais Sata iliokuwa inazidi kudhoofika ilisababisha mgogoro wa nani atakayemrithi rais huyo ndani ya chama tawala cha Patriotic Front ambapo mwezi Agosti rais Sata alimfuta kazi waziri wa sheria Wynter Kabimba, aliyeonekana kama mtu anayefaa kabisa kukirithi kiti hicho.

Kaimu rais wa Zambia Guy Scott na Mkewe Charlotte Scott

Kaimu rais wa Zambia Guy Scott na Mkewe Charlotte Scott

Guy Scott hawezi kuwa rais wa Zambia

Kwa upande mwengine Kaimu rais wa Zambia Guy Scott hawezi kuwa rais kwa sababu wazazi wake wanatokea Scottland. Kulingana na katiba ya Zambia, rais wa nchi hiyo ni lazima awe mzambia kamili kwa maana ya kwamba wazazi wake wote wawili wanapaswa kuwa wamezaliwa nchini humo.

Rais Michael Sata alizaliwa katika eneo moja la Kaskazini lijulikanalo kama Mpika mwaka 1937. Alianza kazi yake ya kwanza kama afisa wa polisi, baadaye akaajiriwa kama mfanyakazi wa reli na kisha mwanachama wa chama cha wafanyakazi.

Baada ya Uhuru wa mwaka 1964, Sata alijiunga na chama tawala cha muungano wa kitaifa wa Uhuru yani United National Independence Party na kuwa gavana wa mji mkuu Lusaka katika miaka ya 80. Alijulikana sana wakati huo kama mchapa kazi na alikuwa akichangia pia kwa kusafisha bara bara yeye mwenyewe.

Rais wa Zambia Michael Sata

Rais wa Zambia Michael Sata

Baadaye akajitenga na rais wa kwanza baada ya kupatikana Uhuru Kenneth Kaunda, na kujiunga na vuguvugu la demokrasia ya vyama vingi, Movement for Multi-Party democracy, (MMD) ambayo kampeni ya vuguvugu hilo ilichangia kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka wa 1991.

Chini ya serikali ya MMD, Sata alihudumu kama waziri wa serikali mitaa, kazi, afya, na pia kama waziri asiyekuwa na wizara maalum. Mwaka wa 2001 aliunda chama chake cha Patriotic Front, kilichoshinda uchaguzi wa mwaka 2011 kwa takriban asilimia 42 ya kura.

Sata alijulikana kwa jina la Utani kama King Cobra kutokana na maneno yake makali, kuwakemea mawaziri wake hadharani na kuwahi pia kumuita rais wa zamani wa Marekani George W Bush kuwa kijana mdogo aliye mkoloni wakati alipochelewa kuwasili katika mkutano wao.

Sata pia alishutumiwa na wakosoaji wake kwa kuongoza kimabavu na kuukandamiza upinzani na hata vyombo vya habari.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Sauti na Vidio Kuhusu Mada