Guterres aongoza kura katibu mkuu mpya UN | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Guterres aongoza kura katibu mkuu mpya UN

Waziri mkuu wa zamani wa Ureno Antonio Guterres anaongoza katika kuwania nafasi ya katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kufuatia kura ya siri. Haya yanajiri wakati kuna msukumo wa kutaka kiongozi ajaye awe mwanamke.

USA Antonio Guterres in New York

Antonio Guterres akihutubu

Kura ya kwanza isiyo rasmi jana ya kumchagua kiongozi mwengine wa Umoja wa Mataifa imemuweka aliyekuwa waziri mkuu wa Ureno, Antonio Guterres, kileleni akifuatiwa kwa karibu na rais wa zamani wa Slovenia Danilo Turk, wamesema wanadiplomasia.#bb#

Kura hiyo ya siri iliyopigwa na mabalozi wa Umoja wa Mataifa katika baraza la usalama la umoja huo, iliwaorodhesha wagombea na kura zilizoonyesha iwapo wanawaunga mkono, wanawapinga au hawana maoni.

Wanadiplomasia waliozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, wamesema Guterres alijinyakulia kura kumi na mbili za wanaomuunga mkono na tatu za wasio na maoni kumuhusu.

Guterras alikuwa waziri mkuu wa Ureno kutoka mwaka wa 1995 hadi 2002 na akahudumu kama Kamishna mkuu Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia masuala ya wakimbizi hadi mwishoni mwa mwaka jana. Waziri huyo mkuu wa zamani mwenye umri wa miaka 67 anazungumza Kireno, Kiingereza, Kihispania na Kifaransa kwa ufasaha.

Turk anaetokea Slovenia aliichukua nafasi ya pili kwa kupata kura 11 za kumuunga mkono na alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter, kwamba, amefurahia kwa kutambuliwa, kueleweka na kuungwa mkono na mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Irina Bokowa Generaldirektorin der UNESCO

Irina Bokova alishika nafasi ya tatu

Nafasi ya tatu ilishuhudia mkuu wa UNESCO Irina Bokova wa Bulgaria, waziri wa mambo ya nje wa kitambo wa Macedonia Srgjan Kerim na Vuk Jeremic, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Serbia, wakipata kura sawia.

Mara baada ya kura hiyo kupigwa, balozi wa Japan katika Umoja wa Mataifa Koro Bessho, aliwahutubia wanahabari na kuthibitisha awamu ya kwanza ya kura isiyo rasmi ya kumchagua katibu mkuu mwengine imefanyika. Bessho aidha alisema wagombea watajulishwa matokeo kupitia wawakilishi wa kudumu wa mataifa yaliyowateua.

"Kama mjuavyo tofauti na hapo awali, tumekuwa na mikutano na wagombea wote, tumemaliza hayo na kutokana na hilo tumeandaa kura hii isiyo rasmi. Kura hii ni ya kuwaonyesha wagombea pale wanaposimama katika kinyang'anyiro hiki na pia ni ya kuwafahamisha wanachama wa baraza la usalama mwelekeo utakaochukua mchakato huu," alisema Bessho.

Wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wamekuwa wakipata shinikizo kutoka kwa zaidi ya robo ya mataifa wanachama wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kumchagua katibu mkuu wa kwanza mwanamke. Nusu ya wagombea wanaowania kiti hicho kwa sasa ni wanawake.

Wanachama hao pia wanapata shinikizo la kuchagua mgombea kutoka Ulaya Mashariki, kwani ndilo eneo la pekee ambalo halijatoa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Jacob Safari AP/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com