1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres ahutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Isaac Gamba
25 Septemba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameilezea hali halisi ya ulimwengu hivi sasa wakati akihutubia mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kutoa wito wa ushirikiano badala ya utengano

https://p.dw.com/p/35Rlr
UN-Vollversammlung verurteilt Israel für Gewalt im Gazastreifen
Picha: picture-alliance/Xinhua/Li Muzi

Akizungumzia kwa ufupi juu ya hotuba hiyo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, msemaji wa Umoja wa Mataifa  Farhan Haq alisema Guterres pia atazungumzia kuhusu masuala  yanayohusiana na mabadiliko ya tabia nchi na kusisitiza kuwa watu wote lazima wanufaike na tekinolojia mpya.

Aidha atatoa mwito kwa viongozi wa kidunia juu ya haja ya kushikamana  kwa ajili ya kudumisha amani pamoja na kuheshimu haki za binadamu.

Jumla ya viongozi 133 wa dunia wanatarajia kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa  baraza kuu la Umoja wa Mataifa utakaomalizika Oktoba 1, likiwa ni ongezeko kulinganisha na viongozi 114 waliohudhuria mkutano wa mwaka jana. Hata hivyo nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zitawakilishwa katika mkutano huo na baadhi yake zikiwakilishwa na mawaziri.

Katika kuelekea  mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekuwa akizungumzia dhidi ya kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo, na haja ya kufanyika mageuzi katika siasa za kimataifa hususan katika kipindi hiki ambacho hayajawahi kuhitajika kama yanavyohitajika sasa.

Schweiz - UN-Generalsekretär in Genf
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio GuterresPicha: picture-alliance/Keystone/C. Zingaro

 

Trump kuhutubia mkutano huo

Viongozi wanaofuta siasa kali za kizalendo wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na rais Donald Trump wa Marekani, rais wa Poland Andrzej Duda, waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte pamoja na mawaziri wa mambo ya nje wa Hungary na Austria.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley aliwaeleza waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa rais Donald Trump anayepigia upatu sera ya " Marekani  Kwanza" atazungumzia juu ya kulinda utaifa wa Marekani  wakati atakapohutubia mkutano huo muda mfupi mara baada ya Guterres kutoa hotuba yake.

Wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kujadili amani sambamba  na kuadhimisha miaka 100 ya kiongozi aliyeoongoza harakati za kupinga ubaguzi nchini Afrika Kusini hayati Nelson Mandela waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi alionya kuwa siasa kali za kizalendo na sera za kuyahami masoko  zinazidi kuongezeka.

China na Marekani katika miezi ya  hivi karibuni zimekuwa  katika hali ya vita ya kibiashara huku nchi zote mbili zikitoza viwango vikubwa vya kodi kwa bidhaa kutoka pande zote mbili.

Masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na yale yanayohusiana na migogoro, maeneo yanayokabiliwa na wasiwasi wa kiusalama yanatarajiwa kujadiliwa pembezoni mwa mkutano huo wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

Mgogoro wa Syria uliodumu  miaka saba sasa, mgogoro wa Yemen uliosababisha janga la kibinadamu pamoja na maeneo mengine barani Afrika yaliyo katika wasiwasi wa kiusalama ikiwa ni pamoja na Libya, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati , Mali na Congo huenda pia yakachukua nafasi  katika mkutano huo.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE

Mhariri: Bruce Amani