1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Guterres ahofia kuenea kwa vita vya Ukraine

7 Februari 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea hofu yake, kwamba vita vya Ukraine vinaweza kusambaa zaidi, na kuonya kwamba fursa ya kupata amani inafifia.

https://p.dw.com/p/4NB0k
UN-Generalsekretär Antonio Guterres
Picha: Selcuk Acar/AA/picture alliance

Guterres ameyasema hayo wakati akilihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, siku chache kabla ya kutimia mwaka mmoja tangu Urusi ilipoanzisha vita dhidi yaUkraine.

Katibu mkuu huyo amesema vita hivyo vimesababisha mateso yasiyosemeka kwa watu wa Ukraine, na vinaambatana na athari kubwa kwa dunia nzima. Antonio Guterres amesema dunia inaelekea katika vita vipana bila kujitambua, huku umwagaji wa damu ukizidi kuongezeka.

Amekemea vitisho vya kutumia silaha za maangamizi, akisema kinachozungumzwa na Urusi kuhusu matumizi ya nyuklia ya kimkakati hakiingii akilini. Kiongozi huyo ametahadharisha kwamba hatari kubwa ya kinyuklia inaweza kutokea kwa makusudi au kwa ajali.