1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aendelea na ziara yake barani Afrika

2 Mei 2022

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewatolea mwito watawala wa kijeshi katika nchi za Afrika Magharibi, BurkinaFaso, Guinea na Mali kurudisha madaraka mikononi mwa serikali za kiraia haraka iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/4AjpO
Generalsekretär der Vereinten Nationen Antonio Guterres
Picha: Andrew Kelly/REUTERS

Antonio Guterres pamoja na kuzungumzia hali katika nchi hizo zinazoshikiliwa na majenerali wa kijeshi aliukumbusha pia ulimwengu kuhusu haja ya kutimiza ahadi za kukabiliana na dharura ya kimazingira. Baada ya kukutana na rais wa Senegal Macky Sall mjini Dakar Guterres alisema wamekubaliana kuhusu haja ya kuendelea kwa mazungumzo na tawala za kijeshi zilizotwaa madaraka kwa nguvu katika nchi hizo tatu za Mali,Guinea na BurkinaFaso ili kuzishawishi kurudisha serikali za kikatiba.

"Kuhusu kanda ya Afrika Magharibi na Sahel tumezungumza kuhusu juhudi za pamoja dhidi ya Ugaidi na machafuko ya makundi ya itikadi kali na pia kuhusu hali katika nchi za BurkinaFaso,Guinea na Mali.Na kuhusiana na hilo tumekubaliana juu ya umuhimu wa kuendelea na mazungumzo na tawala za kijeshi za nchi hizo tatu kuhakikisha zinarudisha utawala wa kidemokrasia haraka iwezekanavyo''

Nchi zote hizo tatu zinakabiliana na uasi wa makundi ya jihad katika ukanda wa Sahel na hivi karibuni zimeshuhudia mapinduzi ya kijeshi ,nchini Mali wanajeshi walitwaa madaraka mnamo mwezi Agosti mwaka 2020 na Mei 2021 wakati Guinea nayo ikitwaliwa na jeshi Septemba mwaka 2021 na huko BurkinaFaso wanajeshi walipindua madarakani serikali na kutwaa madaraka mnamo Januari mwaka 2022.

Bundespräsident Steinmeier im Senegal | Präsident Macky Sall
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mwenzake wa senegal Macky SallPicha: SEYLLOU/AFP

Rais wa Senegal Macky Sall ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS ambayo ilizisimamisha nchi hizo uanachama lakini pia ikaiwekea vikwazo vikali Mali mnamo mwezi Januari baada ya utawala huo kukataa hatua ya kurudi haraka kwenye utawala wa Kiraia.

ECOWAS imetishia pia kuchukua hatua kama hizo dhidi ya Guiena na BurkinaFaso endapo zitashindwa kurudisha uongozi wa kiraia ndani ya kipindi kilichotolewa. Japokuwa tawala za kijeshi za nchi hizo mbili nazo pia zimekataa ratiba zilizotolewa na jumuiya hiyo. Jumatatu wiki iliyopita BurkinaFaso ilisema haina mpango wowote wa kufupisha kipindi cha mpito cha  miaka  mitatu walichokitangazaUfaransa na nchi za Sahel kutathmini vita dhidi ya makundi ya kigaidi. Na Jumamosi jioni kiongozi wa kijeshi huko Guinea Kanali Mamady Doumbouya akatangaza kipindi cha mpito cha miezi 39 ambacho kikimaliza ndipo atakaporudisha utawala wa kiraia.Uamuzi wake huo ulikosolewa sana jana Jumapili na viongozi wa upinzani nchini Guinea ikiwemo kutoka chama cha rais aliyepinduliwa Alpha Conde na makundi ya upinzani yaliyokuwa hayamtaki rais huyo.

Aidha, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amegusia suala la ongezeko la joto duniani akisema dharura ya kimazingira inaongeza hatari ya kiusalama duniani.  Amezitaja nchi za Afrika kwamba mara nyingi  ni wahanga wa mwanzo   wa ongezeko hilo la joto duniani japokuwa hazihusiki katika kusababisha hali hiyo. Nchi zilizoendelea ziliahidi kuyasaidia mataifa hayo ya Kusini kifedha kuelekea hatua ya kuingia katika nishati mbadala zisizochafua mazingira na shughuli za utunzaji mazingira.Sasa katibu mkuu Guterres amesema huu ni wakati wa hatua kuchukuliwa kutimiza ahadi ya kutolewa dolla bilioni 100 kila mwaka kama ilivyotangazwa Paris.