Guinea-Bissau:ECOWAS imelitolea mwito jeshi kubaki kando na siasa | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Guinea-Bissau:ECOWAS imelitolea mwito jeshi kubaki kando na siasa

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS imelitolea mwito jeshi la Guinea-Bissau kutoingilia kati mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Rais mpya wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo akiapishwa mjini Bissau

Rais mpya wa Guinea-Bissau, Umaro Sissoco Embalo akiapishwa mjini Bissau

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS imelitolea mwito jeshi la Guinea-Bissau kutoingilia kati mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini humo, miezi miwili baada ya uchaguzi wa rais uliompa ushindi mgombea wa upinzani. Wiki iliopita nchi hiyo ndogo ya Afrika magharibi ilijikuta na marais wawili na mawaziri wakuu wawili ambao waliapishwa mjini Bissau.

Hali ya sitofahamu inaendelea nchini Guinea-Bissau baada ya marais wawili kuapishwa na kila mmoja kuteuwa waziri mkuu wake. Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS imetowa wito wa kusitishwa mvutano huo na kulionya jeshi kubaki kando na siasa. Kwenye taarifa yake ECOWAS imesema inafuatilia na wasiwasi mkubwa hali inayoendelea hivi sasa nchini humo wakati ambapo koti kuu ikisubiriwa kutoa uamzi wake kuhusu malamiko ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Toka ijumaa jeshi lilionekana kwenye mji mkuu Bissau, likizingira baadhi ya majengo ya serikali, ikiwemo redio na runinga ya taifa, bila kufahamu ikiwa linaunga mkono upande upi. Waziri mkuu wa zamani Domingos Simoes Pereira, mgombea wa chama kikuu cha PAIGC amepinga ushindi wa mgombea wa mpinzani Umaro Sissoco Embalo.

Guinea-Bissau na marais wawili na mawaziri wakuu wawili kufuatia utata wa matokeo ya uchaguzi.

Guinea-Bissau na marais wawili na mawaziri wakuu wawili kufuatia utata wa matokeo ya uchaguzi.

Alkhamisi Umaro Embalo aliapishwa kuwa rais baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo mwezi januari. Hivi sasa yeye ndio alieko ikulu, na Ijumaa alimteuwa Nuno Gomes Nabiam kama waziri mkuu wake.

Kwenye rafla ya kuapishwa kwake waziri mkuu mpya Gomes alisema kwamba majukumu yake ya kwanza ni kuhakikisha amani na usalama wa wananchi wake.

''Ninaimani kwamba serikali hii itasaidia raia wa Guinea-Bissau kwa usalama wa jamii na usalama wa mali zao''alisema Gomes.

Kwa upande wake chama cha PAIGC chenye uwingi wa viti bungeni, kilimuapisha spika wa bunge kuwa rais wa mpito hadi hapo koti kuu itakapo toa uamzi wake kuhusu matokeo ya tume ya uchaguzi.

Soma zaidi:Uchaguzi Guinea Bissau mtafaruku mtupu

Lakini bwana Domingos Pereira ,wa chama cha PAIGC, kilichoiongoza Guinea-Bissau kupata uhuru wake na kilichokuwa chama pekee mpaka 1990, alikataa kuapishwa kwa Embaló, akisema uchaguzi ulikuwa na udanganyifu.

Uamzi wa koti kuu wajaa na utata 

Huku hayo yakiendelea mahakama ya juu ya nchi hiyo ilitoa  uamuzi kuhusu ombi la kubatilisha ushindi wa Embaló. Uamzi huo mwenye utata mwingi haukufafanua ikiwa uchaguzi urejewe ao hapana.

Kura zilikusudiwa kufuta kumbukumbu ya yaliyopita, lakini badala yake, zimesababisha mgogoro mpya wa kisiasa katika taifa ambalo Jeshi limekuwa na ushawishi wa kisiasa.Tume ya uchaguzi nchini humo ilimtangaza bwana Embaló kuwa amemshinda mpinzani wake, Domingos Simoes Pereira kwa asilimia 54% kwa 46% katika uchaguzi wa duru ya pili mwezi Desemba tarehe 29.

Guinea-Bissau imeshuhudia matukio tisa ya mapinduzi tangu mwaka 1980.Koloni hilo la zamani la Ureno, pia limekuwa njia ya usafirishaji wa madawa ya kulevya kutoka Amerika Kusini yakielekea Ulaya.