Guardiola asalimu amri kinyang′anyiro cha ubingwa | Michezo | DW | 16.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Premier League

Guardiola asalimu amri kinyang'anyiro cha ubingwa

Matumaini ya Manchester City kutwaa taji la Premier League yamepata pigo kubwa jana baada ya Everton kuwaduwaza kwa kuwafunga mabao manne kwa sifuri.

 Kilikuwa kichapo kibaya zaidi kuwahi kumkumba kocha Pep Guardiola katika ligi. Na baada ya kichapo hicho, Guardiola alikiri kuwa City sasa hawako tena kwenye kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi.

City sasa wako katika nafasi ya tano, na pengo la pointi kumi nyuma ya vinara Chelsea. Chelsea walirejesha pengo la pointi saba kileleni baada ya ushindi wa 3.0 dhidi ya Leicester City. Tottenham Hotspurs wako katika nafasi ya pili na pointi 45 baada ya ushindi wa 4-0 dhidi ya West Bromwich Albion.

Liverpool wako katika nafasi ya tatu pointi sawa na Spurs kutokana na sare yao ya bao moja kwa moja na Manchester United. Arsenal ni wa nne na pointi 42 baada ya kuwaangamiza washika mkia Swansea 4-0.

Nchini Uhispania, Sevilla iliizuia Real Madrid kushinda mchuano wa 41 mfululizo baada ya kuifunga 2-1 hapo jana na kuwakaribia mahasimu hao katika nafasi ya pili na tofauti ya pointi moja tu. Barcelona walibakia katika nafasi ya tatu pointi mbili nyuma ya Madrid, baada ya kuwazaba Las Palmas 5-0. Nambari nne Atletico Madrid waliwafunga Real Betis moja bila na wako nyuma ya vinara na pengo la pointi sita. Madrid hata hivyo wana mchuano mmoja wa ziada

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com