Ghasia zaendelea Misri | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ghasia zaendelea Misri

Ghasia zinazoendelea nchini Misri kati ya wafuasi wa kiongozi aliyeondolewa madarakani, Mohammed Mursi na wale wanaompinga, zimesababisha mauaji ya mtu mmoja mapema leo asubuhi.

Waandamanaji mjini Cairo

Waandamanaji mjini Cairo

Mauaji hayo yamefanyika baada ya rais wa mpito, Adli Mansour kuwaomba Wamisri wapatane. Taarifa zilizotolewa kwenye mtandao wa habari unaomilikiwa na serikali wa Al-Ahram, zimeeleza kuwa mtu huyo ameuawa katika shambulio dhidi ya mamia ya waandamanaji wanaomuunga mkono Mursi karibu na chuo kikuu cha Cairo, huku watu wengine 15 wakiwa wamejeruhiwa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi kwa lengo la kutuliza ghasia hizo, ambazo zimesababisha magari kadhaa kuharibiwa vibaya pamoja na kuchomwa moto.

Duru za kipolisi zimeeleza kuwa mamia ya wafuasi wa Mursi walipambana na wakaazi wa eneo hilo, wauza bidhaa mitaani pamoja na watu wengine karibu na chuo kikuu cha Cairo katika jimbo la Giza. Polisi wamesema kuwa risasi zilifyatuliwa na mawe yalirushwa wakati wa tukio hilo.

Udugu wa Kiislamu wadai watu watano wameuwa

Hata hivyo, chama cha Udugu wa Kiislamu kimeandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, kwamba watu watano wameuawa katika ghasia za leo.

Ghasia nyingine zilitokea jana Jumatatu na kusababisha mauaji ya watu wanne na wengine 28 walijeruhiwa. Mauaji hayo yalitokea wakati wafuasi wa Mursi walipoukaribia uwanja wa Tahrir, ambako wapinzani wake walikuwa wakifanya maandamano.

Rais wa Misri, Adli Mansour

Rais wa Misri, Adli Mansour

Mauaji ya leo yametokea wakati ambapo Rais wa mpito wa Misri, Adli Mansour kutoa wito wa kuwepo maridhiano miongoni mwa Wamisri. Akihutubia kupitia televisheni wakati wa kuadhimisha kumbukumbu ya mapinduzi ya Misri ya mwaka 1952, ya kuuondoa utawala wa kifalme, Mansour amesema wanataka kufungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hiyo.

Misri, leo inaadhimisha miaka 61 tangu kufanyika kwa mapinduzi hayo Julai 23, baada ya kuondolewa kwa utawala wa kifalme uliodumu kwa miaka 150. Mapinduzi hayo yalifanywa na maafisa huru, akiwemo rais wa zamani, Gamal Abdel Nasser na Jenerali Mohamed Naguib.

Muda wa kuijenga upya Misri, umewadia

Mansour amesema umewadia muda muafaka wa kuijenga upya Misri ambayo imeachana na mambo yaliyopita kwa lengo la kuujenga mustakabali wa baadae wa nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa mpito wa Misri alichukua madaraka ya Misri, tarehe 4 ya mwezi huu wa Julai, siku moja baada ya Mursi, mwanachama wa Udugu wa Kiislamu, kuondolewa madarakani na jeshi, huku kukiwa na maandamano ya kumtaka aondoke madarakani.

Mohammed Mursi

Mohammed Mursi

Mauaji ya jana yalifanyika muda mfupi baada ya familia ya Mursi kumtuhumu mkuu wa jeshi la Misri, Abdel Fattah al-Sissi kwa kumteka nyara Mursi, ambaye hadi sasa hajaonekana tangu alipopinduliwa kijeshi. Mtoto wa kiume wa Mursi, Osama, amesema familia yake haijui mahali alipo Mursi na hawajaweza kuwasiliana nae.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo, Osama amesema wanamtuhumu Al-Sissi na kundi lake ambalo limeunga mkono mapinduzi ya kijeshi na kuwateka nyara raia pamoja na aliyekuwa rais wa nchi hiyo.

Marekani na Umoja wa Ulaya, zimewataka viongozi wa mpito wa Misri, kumuachia Mursi. Wafuasi wa Mursi wamekuwa wakiandamana mjini Cairo, tangu kupinduliwa kwa kiongozi huyo na wamesema wataendelea na maandamano hadi kiongozi huyo atakaporejeshwa madarakani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,DPAE
Mhariri: Josephat Charo

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com