Gharama ya maji yapanda mjini Nairobi | Masuala ya Jamii | DW | 27.08.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Gharama ya maji yapanda mjini Nairobi

Mgao wa maji mara moja kwa wiki

default

Tatizo la maji laongezeka katika vitongoji vya Nairobi

Maji yamekuwa kitu cha thamani kubwa mjini Nairobi Kenya kufuatia kipindi kirefu cha ukame ambacho kimesababisha maji katika mabwawa ya kuhifadhia maji kukauka. Hali hii imeilazimu seriklia ya Kenya kuchukua hatua za haraka kukabiliana nayo. Vitongoji vingi vya mji mkuu Nairobi hupata maji mara moja kwa wiki na hata mara nyingine kukosa kabisa. Katika mitaa ya madongo-poromoka, ambako hakuna mifumo ya ugavi wa maji, watu wengi hawawezi kugharamia maji.

Katika eneo la madongo-poromoka la Kangemi, watu wengi wamesimama kwenye foleni ndefu wakisuburi kununua maji. Muuzaji maji katika kituo hicho, Paul Mwangi, anawajazia maji na kuwauzia kwa bei ya chini kabisa. Kila chombo anakiuza shilingi tatu za Kenya. Katika maeneo mengine ya mji mkuu Nairobi watu wanalazimika kulipa shilingi 20 au hata zaidi, gharama ambayo ni kubwa kwa watu ambao tayari wanaishi chini ya kiwango cha shilingi 100 za Kenya kwa siku. Hata bwana Paul Mwangi huenda asiweze kuendelea kuyauza maji kwa bei yake hiyo ya shilingi tatu kwa muda mrefu. Maji hayo analetewa na idra ya serikali inayohusika na usambazaji wa maji mjini Nairobi na kodi anayolipa inaendelea kupanda.

Gharama ya maji mjini Nairobi imepanda sana kufuatia kipindi kirefu cha ukame kilichosababisha mito kukauka. Kwa sasa maji mengi yanapatikana kutoka kwenye visima. Serikali imeanzisha mgao wa maji katika mji mzima wa Nairobi, huku maji yakisambazwa kupitia mifereji mara moja kwa wiki. Vinginevyo watu wanalazimika kutegemea maji waliyonayo na kuyatumia kwa uangalifu mkubwa isije wakajikuta kwenye shida ya kutokuwa na hata ya kunywa. Ni wakati mgumu kwa wakaazi wa Nairobi lakini ni mazingira ya wala riba kunufaika.

Wakaazi wa mtaa wa Kangemi wanalazimika kila siku kuilalamikia wizara ya maji, lakini hawana muda wa kufanya hivyo kwani wana shughuli nyingine muhimu za kufanya kujikimu kimaisha, anasema Sylvia Ndikila, mkaazi wa Kangemi.

„Kwa sababu watu wanakwenda mbali sana kutafuta maji. Unataka kufua nguo lakini hakuna maji. Pengine umepata ndoo mbili tu kutoka mbali huwezi kufua. Maji hayo ni ya kupikia tu, kuoshea vyombo na kazi kama hizo.“

Maji yanakosekana pia hata katika shule. Ingawa wanafunzi wanapata chakula cha mchana kama kawaida, mara nyengine wanakosa kutokana na tatizo la maji. Vyoo katika shule haviwezi kusafishwa pamoja na vyoo vya umma vilivyoko karibu na kituo cha kuuzia maji cha Kangemi. Vyoo hivi vinatumiwa na mamia ya watu, lakini kutokana na uhaba wa maji, watu wanalazimika kujisaidia mahala pengine maana msalani hakwendeki tena. Huyu hapa mkaazi wa mtaa wa Kangemi.

„Watu wengi hutumia mifuko na kisha kuitupa ovyo. Unaweza kufikiria vipi tabia hiyo ilivyo hatari, kuona kinyeshi kwenye mifuko katika mazingira yetu“

Mifuko hiyo ya plastiki imepewa jina la vyoo vya kupaa. Katika mtaa wa Kangemi kuna harufu nzito inayodhihirisha kwamba mifuko hii inatumika sana. Bwana Paul Mwangi, anayeuza maji huko Kangemi ana furaha kwamba kwa maji anayoyauza, anaweza kuwasaidia majirani zake, lakini anahisi hana uwezo wa kusaidia zaidi.

Iwapo hali itaendlelea kama ilivyo hivi sasa, uhaba wa maji mjini Nairobi utazusha matatizo ya kiafya katika siku zijazo. Tayari kuna taarifa kwamba watoto wengi katika mtaa wa mabanda wa Kangemi wamepelekwa katika vituo vya afya kutokana na matatizo ya kuendesha.

Mwandishi Diekhans, Antje/Josephat Charo

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.08.2009
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JJde
 • Tarehe 27.08.2009
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JJde
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com