1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghana yawapa hifadhi wafungwa wa Guantanamo

Admin.WagnerD7 Januari 2016

Wanaume wawili waliokamatwa nchini Afghanistan na kuzuiliwa katika gereza la Marekani la Guantanamo liliko nchini Cuba, kwa miaka14 bila kufunguliwa mashtaka wameachiliwa huru na kupelekwa Ghana kuanza maisha mapya.

https://p.dw.com/p/1HZbL
Symbolbild Guantanamo
Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Dharapak

Wanaume hao ambao ni raia wa Yemen ni wa kwanza kuachiwa huru katika msururu wa wafungwa wanaotarajiwa kuachiliwa mwezi huu, hii ikiwa ni juhudi ya utawala wa Rais Barak Obama wa Marekani kupunguza idadi ya wafungwa katika gereza hilo na hatimaye kulifunga kabisa kabla ya kumalizika muhula wake wa pili na wa mwisho wa urais mwaka huu.

Wabunge wa chama cha Republican kinacholitawala bunge la Marekani wanapinga azma ya Obama kufunga gereza hilo na kuwapa hifadhi wafungwa hao ndani ya ardhi ya Marekani. Kufika sasa kuna wafungwa 105 wanaozuiliwa katika kambi hiyo ya jeshi la Marekani miongoni mwao wafungwa 50 amabao wamepewa ithibati ya kuwachiwa huru.

Wanaume hao, Mahmud Umar Muhammad Bin Atef na Khalid Muhammad Salih Al-Dhuby, walizuliwa kama wanamgambo hatari ambao walituhumiwa kupata mafunzo ya kundi la al-Qaida na hatimaye kupigana upande wa Taliban.

Wawili hao walikuwa wameaachiwa tangu mwaka 2009 lakini Marekani haikuweza kuwapeleka wafungwa wa Guantanamo nchini Yemen kufuatia hali tete iliyokuwa nchini humo wakati huo na badala yake kutafutiwa taifa ambalo lingekubali kuwapatia hifadhi. Ghana watatoa hifadhi kwa muda

Symbolbild Guantanamo
Picha: Getty Images/J. Moore

Nyaraka za kijeshi zinasema kuwa wanaume hao ambao wako katika miaka yao ya thalathini walikulia Saudi Arabia na baadae wakajiunga na kundi la kigaidi na kwenda kupata mafunzo na kushiriki mapigano nchini Afghanistan. Ushahidi unaonesha kuwa Bin Atef alijeruhiwa vibaya katika shambulizi lililofanyika kaskazini mwa Afghanistan karibu na eneo la Mazar-e-sharif katika mapigano ambayo afisa mmoja wa CIA aliuliwa. Bin Atef pia alikuwa kiongozi muhimu katika mashambulizi makali yaliyozuka baina ya maafisa wa gereza la Guantanamo na wafungwa mwaka 2007.

Ghana, ambayo haijawahi kuwapa hifadhi wafungwa wa Guantanamo, imedokeza kuwa wawili hao watapewa hifadhi ya muda, hayo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo.

Taarifa hiyo pia ilidokeza kwamba Ghana pia imewapatia hifadhi watu wengine wawili ambao walishatakiwa katika mahakama ya kimataifa iliyokuwa ikiendesha kesi za mauji ya kimbari ya Rwanda iliyokuwa na makao yake mjini Arusha, Tanzania.

Wizara ya mambo ya nje ya Ghana pia iliongeza kuwa kutokana na mzozo wa kibinadamu katika eneo la Mashariki ya Kati itatoa nafasi ya hifadhi kwa raia wa Syria walio na jamaa zao nchini humo lakini haikusema idadi kamili itakaowachukua, ingawa imesisitiza kuwa mienendo ya wale watakaopewa hifadhi itafuatiliwa kwa karibu.

Mwandishi: Ambia Hirsi/APE

Mhariri: Mohammed Khelef