Ghana: Mfano wa kuigwa barani Afrika | NRS-Import | DW | 16.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Ghana: Mfano wa kuigwa barani Afrika

Ghana ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizojaaliwa kugundua mafuta katika miaka ya hivi karibuni. Na tokea mwaka wa 2010 Ghana imekuwa inayauza mafuta hayo nje. Jee mafuta hayo yataleta neema kwa nchi hiyo ?

Kiwanda cha mafuta nchini Ghana.

Kiwanda cha mafuta nchini Ghana.

Jee vipi Ghana itaeweza kuepuka kinachoitwa laana ya raslimali ya mafuta ambayo nchi hiyo ilianza kuyauza nje tokea mwaka wa 2010? Jee viongozi wa nchi hiyo, kama wa nchi nyingine zenye mafuta nao pia watakengeushwa na lukuki za fedha zinazoingia bila ya daftari.? Na jee vipi matawi yote ya jamii,majimbo na kwa hivyo wananchi wote wataweza kunufaika na utajiri huo mpya?

Kwa Benjamin Boakye jibu la maswali hayo yote ni wazi! Mtaalamu huyo wa maswala ya uchumi amesema Ghana lazima izifuate sheria zake.Pana sababu kwa nini Ghana inahesabika kuwa nchi imara, na ya mfano wa demokrasia, katika eneo la magharibi mwa Afrika- sehemu isiyokuwa na utulivu.

Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi Boakye kutoka kituo cha sera za nishati cha mjini Accra,amesema sheria mpya za sekta ya mafuta nchini Ghana zinajumlisha taratibu zote za lazima zinazoweza kuchangia katika kuleta maendeleo yanayotarajiwa. Hata hivyo mtaalamu huyo ameleeza kuwa mafanikio yatatokana na utekelezaji wa taratibu hizo.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama.

Rais wa Ghana John Dramani Mahama.

Dhamira ya Ghana
Mara baada ya Ghana kuyagundua mafuta kwenye pwani yake mnamo mwaka wa 2007,nchi hiyo ilidhamiria kufanya kila kitu kwa usahihi. Baada ya mashauriano ya kina na wataalamu wa ndani na wa kutoka duniani kote,Ghana iliupitisha mwongozo kamambe wa taratibu, kwa ajili ya sekta yake hiyo mpya ya uchumi. Sheria mpya juu ya ugawaji wa mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta, inaeleza wazi kabisa ,ni kiasi gani cha mapato hayo, serikali inaweza kutumia na kwa ajili gani.

Sera ya fedha za mafuta katika bajeti ya Rais Pamoja na mengine yote,inahakikisha kwamba mapato yanayotokana na mafuta yanaekezwa katika sekta za uchumi na katika majimbo yaliyomo katika orodha ya mambo ya kipaumbele. Sababu ya kufanya hivyo ni kuuepusha uchumi wa Ghana kunasa katika mtego wa kuitegemea sana sekta ya mafuta na kuzipuuza sekta nyingine za uchumi.

Awali ya yote ,sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa zaidi ya nusu ya watu wa Ghana lazima iendelezwe. Lakini mtaalamu wa masuala ya uchumi Benjamin Boakye amelalamika kwamba ukweli ni mwingine. Boakye aliyapiga darubini matumizi ya serikali ya miaka iliyopita. Ameweza kuziona fedha za mafuta ziliekezwa katika shughuli kadhaa za ujenzi wa barabara lakini ni katika majimbo ambayo tayari yana miundombinu bora,na siyo katika sehemu zilizokusudiwa, ambazo hasa zinavihitaji vitega uchumi. Boakye amesema,mbali na hayo,mapato yanayotokana na mafuta yameingia moja kwa moja katika bajeti ya Rais, aghalabu zaidi kuliko sekta muhimu kama vile ya kilimo.

Mwandishi wa kampuni ya Ujerumani ya kuhimiza biashara ya nje "Germany Trade and Invest" Carsten Ehlers anahofia kwamba kasoro hizo zinaweza kuwa mwanzo wa ufisadi wa kiwango kikubwa katika sekta ya mafuta nchini Ghana.Amesema kiwango kikubwa cha fedha za mafuta kitakuja kutokana na utaratibu wa kuyazingatia mahitaji ya kila sehemu husika.

Magari ya kusafirisha mafuta.

Magari ya kusafirisha mafuta.

Mwanya wa rushwa
Kwa sasa Bunge la Ghana linaijadili sheria ya kuhimiza manufaa kwa wazalendo.Sheria hiyo itapasa kuhakikisha kwamba makampuni ya wazalendo yanashiriki katika sekta ya mafuta,kwanza kwa asilimia tano, na baada ya hapo kwa asilimia isiyopungua 60 hadi 90 ya sehemu ya mapato ya makampuni yote yanayozalisha mafuta nchini Ghana na yale yanayohusika na ugavi wa mafuta.

Mwandishi Ehlers anao wasi wasi hasa kwa kuwa,kwa mujibu wa mswada wa sheria husika,Waziri wa mafuta ataweza kuwachagua wajasiramali wa Ghana jinsi apendavyo .Utaratibu wa kuhimiza ushiriki wa wazalendo,aghalabu umesababisha kuongezeka kwa ufisadi na upendeleo katika nchi nyingine.

Lakini licha ya matatizo yote,mwandishi huyo Ehlers haamini iwapo Ghana itakumbwa na pepo mbaya wa mafuta ,kama inavyotokea katika nchi jirani ya Nigeria.Kwa mujibu wa makisio,kila mwaka dola hadi Bilioni sita zinaibwa kutoka kwenye mapato ya mafuta nchini Nigeria.Ghana bado ni ndogo mno kuweza kukifikia kiwango hicho,amesema Ehlers.Kwa mujibu wa takwimu rasmi,mapato ya Ghana yaliyotokana na mafuta,yalifikia dola milioni mia tano mwaka jana.

Ghana inazalisha mapipa zaidi ya 110,000, lakini bado ni chini ya asilimia10 ya mapipa yanayozalishwa na Nigeria, mzalishaji mkuu wa mafuta barani Afrika.Kiwango cha uzalishaji wa mafuta nchini Ghana kinaondoa wasi wasi wa kile kinachoitwa maradhi ya Uholanzi, amesema Ehlers.

Jamii ya Ghana ni yenye matumaini makubwa kufuatia kugunduliwa kwa mafuta.

Jamii ya Ghana ni yenye matumaini makubwa kufuatia kugunduliwa kwa mafuta.

Mauzo ya maliasilia nchini Uholanzi yaliyosababisha kuongezeka kwa thamani ya sarafu yaliziathiri sekta nyingine za uchumi wa nchi. Mtaalamu wa masuala ya uchumi Benjamin Boakye amesema kwa sasa bado ni vigumu kujua ni kwa kiasi gani, mafuta yameleta manufaa au madhara kwa watu wa Ghana.

Hata hivyo ametilia maanani kwamba angalau nchini Ghana upo mwongozo wa kuonyesha kimsingi, jinsi mapato yanayotokana ya mauzo ya mafuta yanavyoweza kuwanufaisha wote. Lakini Boakye amesema wajibu wa kuhakikisha kwamba mwongozo huo unatekelezwa, haumo katika mikono ya serikali tu. Ameeleza kuwa wanajamii wote wa Ghana wanapaswa kuhakikisha kwamba wanasiasa wanazifuata sheria.

Mwandishi:Borowski,Max
Tafsiri:Mtullya Abdu.
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com