1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza yapambana na hisia za madhila

15 Agosti 2014

Huku makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku nyengine tano yakiingia siku yake ya pili kwenye Ukanda wa Gaza, hali ya kibinaadamu inaelezwa kuwa mbaya kwenye eneo hilo linalofananishwa na "gereza la wazi".

https://p.dw.com/p/1Cv9j
Mtoto wa Kipalestina akibeba godoro lake huku akitoka kwenye vifusi vya nyumba yao iliyoshambuliwa na Israel.
Mtoto wa Kipalestina akibeba godoro lake huku akitoka kwenye vifusi vya nyumba yao iliyoshambuliwa na Israel.Picha: M.Hams/AFP/Getty Images

Baada ya wiki tano za mashambulizi, uharibifu kwenye Ukanda wa Gaza umefikia kiwango kisichoelezeka. Mji umeharibiwa vibaya, hospitali haziwezi tena kuwatibu watu, kuna uhaba wa umeme na watu wanateseka.

Ili kufikia waendako, watu huvuuka mabaki ya majengo, wakapanda na kushuka milima ya vifusi na zege. Kila kitu kimejaa vumbi na hewa imejaa harufu ya mabaki ya miili ya wanaadamu na wanyama, ambayo bado iko chini kwenye vifusi.

Hii ndio Gaza baada ya wiki tano za kushambuliwa. Kipande kiduchu, finyu cha ardhi kisicho na rasilimali, ambacho tangu hapo kilishageuzwa masikini na gereza lililotengwa, hivi leo kinaonekana kama kimepigwa na tetemeko la ardhi.

Lakini hili si janga la kimaumbile, bali ni uharibifu uliopangwa na kutekelezwa na binaadamu, anasema Raji Sourani, mwasisi wa Kituo cha Haki za Binaadamu cha Palestina na mshindi wa tuzo ya mwaka jana ya Haki ya Kuishi.

"Hilo ndilo ambalo tumeligundua kutoka siku ya mwanzo kabisa, kwamba kwa namna ya makusudi na dhamira kabisa, raia walikuwa ndio wanaolengwa. Wao ndio waliokuwa kusudio."

Msiba wa kudumu kwa familia

Familia kadhaa ziliuawa kwa mashambulizi kutokea angani ndani ya nyumba zao. Kwa mfano, baada ya kukimbia mara mbili, kwanza kutoka Beit Lahia kaskazini hadi Shajaiya iliyo mashariki na kisha kwenye kitovu cha mji wa Gaza, familia ya Ibrahim Kilani, Wajerumani wenye asili ya Kipalestina, waliuawa wote kwa pamoja ndani ya jengo walilokimbilia masaa machache tu baada ya kuingia humo.

Licha ya mateso na madhila ya vita, bado vijana wa Kipalestina wanajaribu kutabasamu.
Licha ya mateso na madhila ya vita, bado vijana wa Kipalestina wanajaribu kutabasamu.Picha: DW/Bettina Marx

Dk. Ghassani Abu Sitta, raia wa Uingereza mwenye asili ya Palestina anayeishi Lebanon kwa sasa, yuko kwenye timu maalum ya madaktari wanaosaidia upasuaji kwenye Hospitali Kuu ya Gaza. Daktari huyu ni bingwa wa kutibu majeraha katika maeneo ya vita alisema kinachouma kuliko yote ni namna watoto walivyolengwa kwenye mashambulizi haya.

"Kinachoshitua hapa ni asilimia ya watoto waliojeruhiwa, ambao ndio sehemu kubwa ya majeruhi, na idadi ya watoto waliopoteza familia zao zote."

Hadi sasa, takribani watoto 500 wameshauawa kwenye mashambulizi haya ya Israel, wengi wao wakiwa hata hawajaanza kutambaa. Akiwa baba wa watoto wawili, anasema Dokta Ghassan, hawezi kuacha kuhuzunishwa na jaala ya watoto wa Gaza.

Wakati Misri ikipigania kupatikana kwa makubaliano ya muda mrefu kusitisha mashambulizi dhidi ya Ukanda wa Gaza, itachukuwa muda mrefu zaidi kwa watoto na watu wazima wa Gaza kusahau, na hata muda mwingi zaidi kuweza kusamehe.

Mwandishi: Bettina Marx/Mohammed Khelef
Mhariri: Daniel Gakuba