GATES ZIARANI IRAQ | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

GATES ZIARANI IRAQ

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robet Gates amesema kuwa anakubaliana na mawazo ya kusitisha kwa muda mpango wa kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa nchi hiyo waliyoko Iraq,mara baada ya idadi ya wanajeshi elfu 30 watakaporejeshwa mwezi Julai mwaka huu.


Waziri Gates aliyasema hayo leo hii mwishoni mwa ziara yake ya kushtukiza mjini Baghdad, mara baada ya mkutano wake na kamanda wa jeshi la nchi hiyo huko Iraq Genarali David Petraeus.


Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa hali ya usalama katika mji mkuu wa Bhagdad bado si shwari, kauli ambayo ilithibitishwa na shambulizi la mabomu mawili kwenye gari yaliyopelekea vifo vya watu 11 na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa.


Jeshi la Marekani lenye askari laki moja na elfu 57 lililoko nchini humo liko katika mpango wa kupunguza kutoka brigedi 19 zilizopo hivi sasa hadi 15, ambapo kiasi cha askari elfu 37 wataondoka ifikapo Julai mwaka huu.


Robert Gates hivi karibuni alinukuliwa akisema ya kwamba kupunguzwa kwa jeshi hilo kutaendelea ambapo hadi kufikia mwisho wa mwaka huu kiasi cha askari laki moja watakuwa wamekwishaondoka.


Kamanda wa jeshi la Marekani nchini Iraq, Generali Petraeus alisema hivi karibuni ya kwamba anahitaji muda wa kufanya tathmini ya athari zitakazojitokeza kiusalama nchini Iraq, iwapo hatua ya kupunguza itafikiwa.


Waziri wa Ulinzi wa Marekani amesema kuwa General Petraeus mwezi ujayo atawasilisha mapendekezo yake kwa rais na wakuu wengine wa majeshi nchini humo kabla ya yeye kuwasilisha yake.


Gates aliwasili mjini Baghad jana katika ziara ya kushtukiza ikiwa ni mara ya saba toka alipoteuliwa kushika wafidha huo, ikiwa ni siku chache kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja toka kuongezwa zaidi kwa vikosi vya nchi hiyo nchini Iraq.


Alipokelewa na shambulizi la bomu la kujitoa mhanga lililoua watu 25 katika soko moja kwenye kijiji kiitwacho Yathreb kaskazini mwa Baghdad.


Hapo jana Robert Gates alikuwa na mazungumzo na wakuu wa Iraq, juu ya maendeleo katika kuandaa sheria nchini humo,vile vile alijadiliana nao juu ya aina ya makubalino ya kuwepo kwa majeshi ya nchi hiyo nchini Iraq, halikadhalika mafanikio yalifikiwa mpaka hivi sasa.


Majadiliano yalijikita zaidi katika uwekaji wa sheria kwenye matumizi ya nishati ya mafuta na gesi, na sheria tata uliyopitishwa hivi karibuni ya maridhiano inayotoa nafasi kwa wanachama wa chama cha Saddam Hussein cha Baath kurejea katika utumishi wa umma na kujumuika katika jamii ya kawaida.


Hapo jana Rais Bush alikri ya kwamba Marekani inaangalia uwezekano kwa majeshi yake kuendelea kubakia nchini Iraq kwa miaka kadhaa lakini si kuweka kituo cha kijeshi.


Makubaliano ya kuwepo kwa majeshi ya Marekani nchini Iraq yatachukua nafasi ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya majeshi ya Marekani nchini Iraq ambalo muda wake unamalizika tarehe 31 Decemba.


Wakati huo huo katika mji wa Baquba nchini Iraq wamewekwa katika hali ya tahadhari, mnamo wakati ambapo maelfu ya wakaazi wa mji huo wanafanya maandamano ya kutaka kufukuzwa kazi kwa mkuu wa polisi wa mji huo.


Zaidi ya watu 3500 wameandamana katika mji huo uliyoko kwenye jimbo la Diyala kaskazini mwa Baghdad kutaka mkuu huyo wa polisi General Ghanim al Quraishi afukuzwe kazi.

 • Tarehe 11.02.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D5ub
 • Tarehe 11.02.2008
 • Mwandishi Liongo, Aboubakary Jumaa
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D5ub
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com