Gaddafi aanza kukimbiwa na washirika | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.02.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Gaddafi aanza kukimbiwa na washirika

Hali nchini Libya inazidi kuwa mbaya, huku maafisa kadhaa wa serikali ya Muammar Gaddafi wakizidi kumuacha mkono na wageni wakiikimbia nchi hiyo, huku jumuiya ya kimataifa ikiongeza shinikizo kwa Gaddafi.

Muammar Gaddafi

Muammar Gaddafi

Muammar Gaddafi alikuwa amejijengea taswira ya kiongozi shujaa asiyegusika, asiyetukusika na asiyebabaika. Lakini sasa, kuliko wakati mwengine wote wa historia yake ya miongo minne ya kuitawala Libya, kiongozi huyu anajikuta akikabiliwa na kile alichokuwa hajawahi kukitarajia. Kukataliwa na hata watu wake wa karibu.

Wa karibuni zaidi kumkana Gaddafi hadharani, ni waziri wake wa mambo ya ndani, Abdul Fattah Younis. Katika tangazo lake la jana usiku, Younis alisema kwamba, anajiuzulu rasmi wadhifa huo na anajiunga na waandamanaji, ambao alisema wana madai ya haki.

"Mimi kuanzia sasa sio tena waziri wa mambo ya ndani, bali mwanajeshi ninayesimama upande wa umma." Amesema Younis.

Katika mahojiano ya baadaye na kituo cha televisheni cha Al-Arabiya, Younis alisema kwamba mfuasi mmoja wa Gaddafi alijaribu kumuua, lakini risasi ilimkosa na kumjeruhi jamaa yake. Katika hotuba yake hapo jana, Gaddafi alisema kwamba waandamanaji walikuwa wamemuua waziri huyu wa mambo ya ndani.

Waandamanaji mjini Benghazi

Waandamanaji mjini Benghazi

Katika hatua nyengine, Youssef Sawani ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa wakfu wa mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, amejiuzulu wadhifa wake akipingana na mashambulizi dhidi ya raia.

Katika ujumbe alioutuma kwa shirika la habari la Reuters, Sawani amesema kwamba, amejiuzulu nafasi hiyo kwa kuwa hakubaliani na hatua za serikali ya baba wa bosi wake, inavyowakandamiza waandamanaji.

Taarifa za karibuni za kitabibu na shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, zinaonesha kuwa takribani watu 400 wameshauawa na wanajeshi wanaoshukiwa kuwa vikosi vya serikali, wafuasi na mamluki kutoka nje.

Mauaji mengi zaidi yamefanyika katika mji wa Benghazi, ulio mashariki ya Libya, na ambao umekuwa kitovu cha mapambano dhidi ya utawala wa Gaddafi.

Wafanyakazi wa Kituruki wanaoishi nchini Libya, wakisubiri kuokolewa

Wafanyakazi wa Kituruki wanaoishi nchini Libya, wakisubiri kuokolewa

Wakati huo huo, serikali za nchi kadhaa ulimwenguni zimeeendelea na operesheni ya kuwahamisha raia wao walioko Libya, kuwanusuru na mashambulizi, ambayo sasa yameanza kuwaelekea wageni.

Raia wa Misri na Tunisia wanalalamika kwamba, wafuasi wa Gaddafi wanashambulia, wakiwatuhumu kwamba ndio waliochochea machafuko katika nchi yao.

Baraza la Kijeshi linaloongoza Misri kwa sasa na serikali ya muda ya Tunisia zimepeleka ndege na meli za kuwaondoa raia wao.

India nayo inapanga kuwaondoa raia wake wapatao 18,000 kupitia njia ya bahari. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Nirupama Rao, tayari meli ya India ipo njiani kuelekea mji wa Alexandria na maafisa wamekuwa wakitafuta ruhusa ya Libya kuwaondoa raia wao waliopo Tripoli na Benghazi.

Hatua hii ya India inakuja, huku tayari Uturuki na Urusi zikiwa zimeshaanza kuwaondoa raia wake. Leo hii, ndege yenye zaidi ya Warusi 100 imewasili mjini Moscow ikitokea, ikiwarudisha nyumbani sehemu ya wafanyakazi 500 wa Kirusi wanaofanya kazi katika ujenzi wa reli na visima vya mafuta nchini Libya.

Licha ya hotuba kali ya Gaddafi hapo jana , bado hali ya mambo inazidi kuzorota na dalili za kupoteza udhibiti wa nchi zimeanza kujitokeza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com