Finali ya Kombe la UEFA leo | Michezo | DW | 20.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Finali ya Kombe la UEFA leo

Wapi litaenda Kombe: Bremen au Kiev ?

Bremen bila Diego itatamba leo ?

Bremen bila Diego itatamba leo ?

Wiki kabla ya finali ya champions League-Kombe la klabu bingwa barani Ulaya mjini Roma,Itali kati ya mabingwa Manchester United na FC Barcelona, leo ni finali ya Kombe jengine la Ulaya mjini Istanbul-kombe la UEFA-kombe la shirikisho la dimba la Ulaya kati ya Werder Bremen ya Ujerumani na Shakhtar Donetsk ya Ukraine.Rais wa Ukraine Viktor Yushchenko binafsi atakuwa uwanjani Istanbul kuishangiria timu yake:

Bremen inasaka kombe la kwanza la ulaya kwa timu ya Ujerumani tangu kupita miaka 8 na kombe lao la pili tangu bremen kutwaa kombe la washindi la Ulaya-European Cup winners Cup 1992 na la kwanza msimu huu katika kile kinachoweza kuwa vikombe viwili.Kwani, Bremen imekata pia tiketi ya finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani.Isitoshe, Jumamosi hii, Bremen itacheza na Wolfsburg katika finali ya Bundesliga,kwani ni wao walio na ufunguo iwapo Wolfsburg inayohitaji sare tu isitawazwe mabingwa.

Lakini kuna ufa katika kikosi cha Werder Bremen jioni hii, stadi wao wa Brazil Diego,mlinzi wao Mertesecker wa timu ya taifa ya Ujerumani na hata Almeida hawawezi kucheza.Diego amefungiwa na hii inamuumiza kichwa kocha wao Thomas Schaaf anaebidi leo kumteremsha nahodha wake Frank Baumann kuliokoka jahazi lisizame.Shakhtar Donetsk inatumai leo kuwa timu ya kwanza ya Ukraine, kutwaa Kombe la ulaya na kuhakikisha inafanya hivyo, rais wa Ukraine , Viktor Yuschenko amefunga safari hadi Istanbul,Uturuki kujionea kwa macho yake,Donetsk inaandika historia ya dimba.

Kocha wa Donetsk, Lucescu kutoka Rumania, alishika usukani kuiongoza Donetsk Shakhtar, 2004 kutoka kocha mjerumani Bernd Schuster na tangu wakati huo, amekuwa akivuna mafanikio.Ameitawaza Donetsk mara tatu mabingwa wa Ukraine na kuipatia vikombe 2 vya shirikisho la dimba nchini.Leo jioni anataka kupiga hatua moja zaidi.Anabashiri finali ya leo itakuwa ngumu na kwamba itakua mpambano kati ya kikosi kikali cha washambulizi-Bremen na kile chenye ujanja mwingi na uvumilivu cha Donetsk.Sitapenda kuagua wapi kombe litaelekea-Bremen au Kiev.

Muandishi:Ramadhan Ali/DPAE

Mhariri:M-Abdulrahman