1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yaziondolea makosa Qatar na Urusi

13 Novemba 2014

Shirikisho la kandanda Ulimwenguni – FIFA limeziondolea makosa Qatar na Urusi nchi mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka wa 2018 na 2022 .Nchi hizo sasa zinaendelea na maandalizi

https://p.dw.com/p/1DmUp
Bildergalerie Stadien Fußballweltmeisterschaft 2022 in Katar
Picha: picture alliance/dpa

FIFA imefutilia mbali uwezekano wowote wa kupigwa kura upya ili kuamua kuhusu mwenyeji wa tamasha hilo licha ya kuwepo madai chungu nzima ya ufisadi na udanganyifu.

Ripoti ya kina ya kamati ya nidhamu ya FIFA ilikiri kuwa hata ingawa kulikuwa na msururu wa matukio ya udanganyifu katika mchakato wa kuwasilisha maombi ya kuwa mwenyeji wa dimba la Kombe la Dunia la mwaka wa 2022, pamoja na Kombe la Dunia la mwaka wa 2018 nchini Urusi, hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kutaka kuanzishwa upya mchakato huo.

Ripoti hiyo ilionyesha matukio kadhaa ambayo yalionekana kutilia shaka uhalali wa mchakato wa kutafuta wenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia la mwaka wa 2018 na 2022.

WM 2018 Rußland Vladimir Putin Boykott
Rais wa Urusi Vladimir Putin katika Makao makuu ya FIFAPicha: PHILIPPE DESMAZES/AFP/Getty Images

Ripoti hiyo yenye kurasa 42 iliyozinduliwa na Hans Joachim Eckert, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi, imesema hata hivyo kuwa matukio hayo yalikuwa ni machache mno yasiyotosha kufanywa uamuzi wa kuanzisha tena mfumo wa kuwasilisha maombi ya kuandaa Kombe la Dunia.

Hivyo basi kamati ya nidhamu ya FIFA imeufunga kabisa mchakato huo na Urusi na Qatar zinaweza kuendelea mbele na maandalizi ya mashindano hayo.

Kamati hiyo hata hivyo imependekeza msururu wa mageuzi yanayohitajika kwa ajili ya michakato ijayo ya kuwasilisha maombi ya kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia, katika juhudi za kulinda uhalali wa tamasha hillo la michezo ambalo ni maarufu sana ulimwenguni.

Hiyo ni pamoja kuwekewa mipaka ya miaka minne nyadhifa za Kamati Kuu ya FIFA, Baraza Kuu la FIFA, badala ya kamati kuu, kuamua kuhusu wenyeji wa usoni, mfumo wa wazi wa mzunguko na kupigwa marufuku wanakamati wanaozitembelea nchi zinazowasilisha maombi ya kutaka kuandaa Kombe la Dunia.

Kwingineko, Qatar imesema kuwa iko tayari kusaidia kuwa mwenyeji wa Kinyang'anyiro cha Kombe la Mataifa ya Afrika hapo mwakani 2015, japokuwa haijapokea ombi lolote rasmi.

Sheikh Hamad bin Khalifa bin Ahmed al-Thani amesema katika taarifa kuwa kama Qatar itaombwa kuandaa dimba hilo baada ya Morocco hapo jana kupigwa marufuku na kupokonywa kibali cha kuwa mwenyeji, basi itakubali kwa sababu ya uhusiano mkubwa ilio nao na Rais wa Shirikisho la Kandanda - CAF Issa Hayatou.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu