FIFA yataka Niersbach afungiwe miaka miwili | Michezo | DW | 20.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

FIFA yataka Niersbach afungiwe miaka miwili

Jopo la maamuzi la Kamati ya maadili ya FIFA limependekeza kuwa aliyekuwa rais wa Shirikisho la Kandanda Ujerumani – DFB Wolfgang Niersbach apigwe marufuku ya kujihusisha na shughuli zozote za kandanda kwa miaka miwili

Hatua hiyo ni kuhusiana na kashfa inayozunguka kibali cha nchi hiyo kuandaa Kombe la Dunia mwaka wa 2006. Niersbach, makamu wa rais wa kamati iliyoandaa Kombe la Dunia 2006 na mwanachama wa sasa wa Baraza la FIFA na kamati kuu ya Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA, alijiuzulu Novemba mwaka jana kutoka shirikisho la kandanda la Ujerumani.

Mkuu wa kamati ya maadili ya FIFA alianzisha uchunguzi mwezi Machi na mwezi uliopita akaikabidhi ripoti yake kwa jopo la kufanya maamuzi, ambalo sasa sasa limeamua kuendelea na mchakato rasmi wa kuamua kuhusu kesi ya Niersbach aliye na umri wa miaka 65. Kando na kupigwa marufuku kwa miaka miwili, jopo la uchunguzi pia limependekeza Niersbach atozwe faini ya euro 27,000

Lakini mara tu baada ya taarifa hiyo kutolewa, Niersbach alijibu kwa kusema kuwa atafanya kila liwezekanalo ili kupinga uwezekano wa kuchukuliwa adhabu hiyo. anasema ni suali la heshima na kulinda haki zake za kibinafsi kutumia mbinu zote za kisheria kupinga hatua yoyote dhidi yake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com