1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yapinga kalenda ya Shirikisho la Soka la DRC

Saumu Njama Zuberi Ally
16 Machi 2026

Uchaguzi wa Shirikisho la Soka la DRC umeahirishwa! FIFA yatoa muda zaidi huku mashabiki wakitarajia mabadiliko makubwa katika soka la taifa.

https://p.dw.com/p/5AVRR
Shabiki wa kandanda wa DRC
Kwa muda mrefu soka la Kongo limekumbwa na changamoto za utendaji na uongozi.Picha: Sebastien Bozon/AFP/Getty Images

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FECOFA) uliokuwa umepangwa kufanyika Aprili, na kuupanga upya hadi mwezi Mei. Hatua hii imechukuliwa kufuatia ucheleweshaji wa maandalizi ya uchaguzi, ikiwemo kuchelewa kufunguliwa kwa akaunti ya benki iliyokuwa inakusudiwa kupokea fedha kutoka FIFA kwa ajili ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari, FIFA imependekeza:

"FECOFA iwajulishe mara moja wanachama wake na wadau wote kuhusu kuahirishwa kwa uchaguzi katika ngazi za ligi za kitaifa pamoja na zile za Kamati ya Utendaji. Zaidi ya hayo, tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi ya ugombea, ambayo ilikuwa kumalizika Machi 12, pia itaongezwa."

Historia ya Uongozi wa FECOFA

Tangu 2021, baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa shirikisho, Constant Omary, FECOFA imekuwa ikisimamiwa na kamati za muda zilizoundwa chini ya uangalizi wa FIFA, zinazojulikana kama CONOR.

AFCON 2025 |  DR Kongo
Timu ya taifa ya kandanda ya Kongo.Picha: Themba Hadebe/AP Photo/picture alliance

Ingawa hatua hii ililenga kurekebisha hali, ligi ya soka nchini Kongo imeendelea kukumbwa na changamoto, ikiwa ni pamoja na:

-Mgawanyiko wa ligi kuu katika makundi mawili.

-Ongezeko la idadi ya vilabu, zaidi ya 30 kwenye ligi kuu.

-Baadhi ya vilabu kutokuwa na bajeti ya kutosha kusafirisha wachezaji wao kwenye mechi.

Wafuatiliaji wa soka wanaamini kuwa uchaguzi mpya utaleta uwezo, usawa, na maendeleo ya taswira ya soka la jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. "Soka la Kongo linahitaji watu wenye uelewa na nia ya maendeleo. Wengi hujitokeza kwa maslahi binafsi na kusababisha uchafuzi wa taswira ya soka la nchi hiyo,” alisema Rajabu Juma, shabiki wa soka wa Kongo, katika mahojiano na DW.

Kalenda ya Uchaguzi Mpya

Uchaguzi wa ligi za kitaifa za kandanda (LIFNAJ kwa vijana, LINAFF kwa wanawake, na LINAFOOT kwa ligi kuu) uliopangwa awali Machi 9-11, 2026, umeahirishwa hadi Aprili 6-8.

Uchaguzi wa FECOFA wa kitaifa sasa umepangwa kufanyika mwezi Mei.

Kwa muda mrefu sasa, soka la Kongo limekumbwa na changamoto za utendaji na uongozi, lakini uchaguzi ujao unatarajiwa kuanzisha kipindi kipya cha utawala bora, uwazi, na maendeleo ya michezo nchini.