1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fidel Castro atimiza umri wa miaka 85

12 Agosti 2011
https://p.dw.com/p/Rffe
Fidel Castro (kushoto) na nduguye, rais wa sasa Raul Castro.Picha: picture alliance/dpa

Fidel Castro anayetimiza miaka 85 tarehe 13 Agosti ,aliacha wadhifa wake wa mwisho wa uongozi mwaka huu, alipojiuzulu kama kiongozi wa chama tawala cha kikoministi na kujiondoa taratibu katika shughuli za hadhara

Hatua yake hiyo pia inaelekea kuwa sio tu ni chaguo la lazima bali pia mpango wa mpito wa kuitoa Cuba katika hali ya kuwa utegemea moja kwa moja uongozi wa Fidel maarufu kwa Wacuba kama Commandante.

Kwa sasa ni nadra kuonekana na amejiweka kando huku mdogo wake Raul Castro na aliyechukua nafasi yake kama rais, akijitihadi kuleta mageuzi katika uchumi wa Cuba unaofanana na ule wa enzi ya Kisovieti.

Sherehe za kuadhimisha miaka 85 tangu kuzaliwa Fidel Castro zinafanyika leo, kwa burudani kubwa ya muziki itakayoonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya taifa. Haijafahamika bado ikiwa Castro atahudhuria burudani hiyo.

Castro aliingia madarakani siku ya mwaka mpya 1959, wakati majeshi ya wapiganaji yakitokea milima ya mashariki ya Sierra Maestra yalipouangusha utawala wa Fulgencio Batista ulioungwa mkono na Marekani.

Alipokuwa madarakani Fidel , alishuhudia marais tisa wakitawala Marekani na miongo mitano ya uhasama kati ya nchi yake na dola hilo kuu. Lakini 2006 akafanyiwa uapasuaji wa tumbo na kupata matatizo yalioathiri afya yake.

Fidel alimkabidhi uongozi mdogo wake Raul Castro Februari 2008 na Raul mwenye umri wa miaka 80 akachaguliwa rais na baraza la taifa. Umuhimu wake unaangaliwa kwa mtazamo wa kwamba kwa umbali gani ataongoza njia kuelekea siku za usoni za mapinduzi ya Cuba. Moja linaloangaliwa ni ukosefu wa viongozi vijana chini yake.

Fidel alitokeza wakati wa mkutano mkuu wa chama cha kikoministi mwezi Aprili , akionekana dhaifu na hata kusaidiwa kupanda jukwaani.

Castro alikua maarufu kwa utoaji hotuba ndefu za saa kadhaa, kinyume na nduguye Raul.

Tangu mkutano huo mkuu Fidel ameonekana mara moja katika mkanda wa video akizungumza na kiongozi wa Venezuela Hugo Chavez . Chavez anayetibiwa saratani nchini Cuba ni rafiki wa chanda na pete wa Fidel na mtu anayepepea bendera ya mapinduzi staili ya Cuba nchini mwake na kunadi nadharia hiyo Amerika kusini.

Hadi miezi mitatu iliopita mwana mapinduzi mkongwe Fidel amekua akiandika makala juu ya masuala ya dunia, yaliochapishwa na vyombo vya habari vya Cuba.

Fidel anachukiwa na baadhi lakini anapendwa na wengine. Fundi mmoja wa magari mjini Havana Rafa Marrero alisema " watu walikuwa na wasi wasi nin i kitatokea ikiwa Fidel atakufa, lakini sasa tayari yuko Raul madarakani. Raul alimridhi Fidel, lakini nani atashika nafasi ya Raul atakapoondoka?"

Mchambuzi mmoja anasema si muhimu kama Wacuba wanampenda Fidel Catsro au la, muhimu ni kuwa wanasonga mbele na hiyo ndiyo changamoto kwa Raul Castro katika mpango wake wa kuleta mageuzi.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman / RTRE

Mhariri:Hamidou, Oummilkheir