1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola bilioni 1 zakusanywa kulikarabati kanisa la Notre Dame

Amina Mjahid
17 Aprili 2019

Takriban dola bilioni moja zimeshakusanywa kutoka kwa wachamungu na matajiri wakubwa wa kila pembe ya dunia kwa lengo la kulifanyia ukarabati kanisa kuu mashuhuri la mjini Paris, Notre Dame lililoharibiwa kwa moto.

https://p.dw.com/p/3GxdO
Frankreich Paris | Brand der Kathedrale Notre-Dame de Paris
Picha: Getty Images/AFP/F. Guillot

Wataalam wa ujenzi wamepeleka winchi kubwa na mbao katika eneo la tukio. Maafisa wa zima moto nao bado wanachunguza hasara iliyopatikana na kuona kama nguzo haijaathirika kufuatia janga la moto la jumatatu lililopelekea mnara wa kanisa kuporomoka na kuharibu  paa la kanisa hilo mashuhuri Notre dame.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amezidisha shinikizo alipotangaza muda wa miaka mitano kukamilisha shughuli za kulikarabati kanisa hilo kuu mashuhuri kabisa ulimwenguni lililojengwa karne ya 12.

Frankreich Präsident Macron TV Rede
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/AFP/L. Marin

Rais Macron  anaongoza kikao maalum cha baraza la mawaziri hii leo kuzungumzia msiba wa Notre  Dame ambao wataalam wanaamini ni ajali iliyosababishwa na kazi za ukarabati.

Kengele zitahanikiza kutoka makanisa yote  makuu ya Ufaransa leo usiku kwa hishma ya kanisa hilo kuu mashuhuri.

Maajabu ni kwamba hakuna aliyeuwawa kutokana na janga hilo la moto baada ya maafisa wa zima moto kuwahamisha haraka haraka waumini waliokuwa wakihudhuria misa.

Watu wasiopungua 30 wameshahojiwa na polisi kuhusiana na kadhia hiyo ambayo mwendesha mashitaka wa Paris anasema ni tete na itahitaji muda mrefu

Euro milioni 880 zimeshakusanywa muda mfupi tu tangu janga la moto liliporipuka

Mjumbe maalum wa rais anaeshughulikia turathi za kitamaduni Stephane Bern amekiambia kituo cha matangazo cha France Info zaidi ya Euro milioni 880 (kiwangoa mbacho ni sawa na Dala milioni 995 zimeshakusanywa kwa siku moja na nusu tu tangu janga la moto liliporipuka.

Frankreich Paris | Zerstörung nach Brand der Kathedrale Notre-Dame de Paris
Kanisakuu mashuhuri la mjini Paris, Notre Dame lililoharibiwa kwa motoPicha: Reuters/C. Petit Tesson

Wafadhili wanatokea kila pembe ya dunia  tangu karibu mpaka mbali, matajiri na maskini,kuanzia waachamungu wa kikatoliki na wasio wakatoliki.

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis aliyezungumza kwa simu na rais Macrion jana jioni,amewatolea wito walimwengu wawajibike katika kulijenga upya kanisa kuu la notre dame.

Wakati huo huo muda wa miaka mitano  uliowekwa na rais Macron kukaamilisha shughuli za kulikarabati kanisa Notre dame na ambao unasadifu  wakati mmoja na michezo ya Olympiki ya mwaka 2024 ya mjini Paris unatajwa na wengi kuwa hauwezekani.