1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FAO na maazimio ya kumaliza njaa ulimwenguni.

Scholastica Mazula6 Juni 2008

Mkutano wa Kimataifa wa kuhusu chakula ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula-FAO, uliomalizika jana mjini Roma, umeapa kumaliza tatizo la njaa Ulimwenguni hadi kufikia mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/EEhM
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akiwa na Mkurugenzi wa Shirika la Kilimo na Chakula-FAO Jacques Diouf:Picha: picture-alliance / dpa

Wajumbe katika Mkutano huo wameazimia kuchukua hatua za haraka ili kumaliza mgogoro huo wa chakula ulimwenguni, baada ya mazungumzo yao katika mkutano huo wa Roma.

Katika maazimio yao ya mwisho kiasi cha dola bilioni sita nukta tano ziliahidiwa kutolewa,lakini ambazo zitaelekezwa katika kumaliza tatizo la utumiaji wa mazao kutengeneza mafuta na pia viongozi wote wamekubaliana kusaidia uzalishaji wa chakula katika nchi masikini.

Katika ripoti ya maazimio waliyoitoa, viongozi hao wamesema kwamba wameshawishika kuwa Jumuiya ya Kimataifa inahitaji kuchukua hatua za haraka katika kukabiliana na tatizo lililopo la kupanda kwa bei ya nafaka ulimwenguni na zaidi katika nchi masikini zenye idadi kubwa ya watu.

Shirika la misaada la Oxfam lenye makao yake makuu nchini Uingereza limesema kwamba, Mkutano huo ulikuwa ni hatua muhimu ya kwanza, lakini hautoshi kuweza kumaliza mgogoro huo wa chakula Ulimwenguni.

Mkurugenzi wa Oxfam, Barbara Stocking, ameyasema hayo katika ripoti yake aliyoitoa wakati ambao viongozi kutoka nchi tajiri duniani, wametahadharisha umuhimu wa kutolewa kwa msaada wa kilimo na kwamba mgogoro wa chakula ulimwenguni unahitaji mikakati madhubuti ili kuumaliza.

Bibi Stocking amesema nchi tajiri duniani, zinapaswa kukusanya fedha nyingi zaidi ili kulishughulikia haraka iwezekanavyo tatizo hilo lakini pia kwa kuchukua baadhi ya makusanyo hayo kumaliza tatizo la mafuta utengenezwaji wa mafuta kwa kutumia mazao na kuandaa msaada wa muda mrefu kwa ajili ya kilimo.

Kwa kuzingatia moja ya malengo ya Umoja wa mataifa, mbali na tatizo lililopo,bei za nafaka zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza njaa na ukosefu wa chakula ulimwenguni kitendo kilichotia nguvu Mkutano wa FAO, kuazimia kutosheleza chakula nusu ya watu ambao wanakabiliwa na njaa kali hadi kufikia mwaka 2015.

Taarifa ya FAO, imesema kuwa kunaulazima wa haraka sana wa kuzisaidia nchi zinazoendelea katika kukuza kilimo na kuzalisha chakula kwa wingi ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika pande zote Serikali na hata katika sekta binafsi.

Maendeleo ya kutengeneza mafuta kwa kutumia nafaka, yamekuwa yakiungwa mkono sana katika nchi za Brazil na Marekani, lakini kitendo hicho kimekuwa kikipingwa na wengine kwa sababu ya kutumia nafaka nyingi ambazo zingeweza kutengenezwa kuwa chakula.

Akizungumza mara tu baada ya Mkutano huo, Mkurugenzi wa FAO.Jacques Diof, amethibitisha kuwa kiasi cha dola bilioni sita nukta tano zimeahidiwa kutolewa.

Amesema ahadi ya fedha nyingi zimetolewa na Benki ya maendeleo ya kiislamu ambayo imeahidi kutoa dola bilioni moja nukta tano ambayo ni sawa na ahadi ya Ufaransa, Banki ya dunia dola bilioni moja nukta mbili, wakati Benki ya maendeleo ya Afrika imeahidi kutoa dola bilioni moja.

Kwa mujibu wa Benki kuu ya Dunia, kupanda kwa bei ya chakula kumeongezeka katika kipindi cha miaka mitatu, zaidi katika nchi za Misri na haiti na katika nchi nyingi za Afrika.

Mkutano Kuhusu chakula ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa la kilimo na chakula ulihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi zipatazo mia moja na themanini na moja.