1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Facebook mashakani

Saumu Mwasimba
21 Machi 2018

Aleksander Kogan anayehusishwa na Cambridge Analytica inayoandamwa na sakata la utumiaji wa data za watu kinyume na sheria katika mtandao wa Facebook amesema kwamba usahihi wa taarifa zilizotolewa umeongezwa chumvi.

https://p.dw.com/p/2ugRi
Greoßbritannien Alexander Nix CEO Cambridge Analytica in London
Mkurugenzi mkuu wa Cambridge Analytica(katikati) Alexander NixPicha: Reuters/H. Nicholls

Mhadhiri  wa chuo kikuu cha Cambridge anayehusishwa na kampuni ya Uingereza ya utafiti wa Data ya Cambridge Analytica ambayo iko katikati ya sakata la utumiaji wa data za watu kinyume na sheria katika mtandao wa Facebook amesema kwamba usahihi wa taarifa zilizotolewa umeongezwa chumvi. Aleksander Kogan inadaiwa alitoa data za watu kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na kuzisambaza katika kampuni ya utafiti ya Cambridge Analytica  kuunga mkono kampeini ya Donald Trump katika uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Aleksander Kogan anasema kwamba taarifa kuhusu usahihi wa data alizozikusanya zimeongezwa chumvi kupita kiasi na kwamba katika kisa hiki amegeuzwa kuwa mbuzi wa kafara na mtandao huo wa kijamii wa Facebook pamoja na kampuni ya ushauri wa masuala ya kisiasa ya Uingereza. Akihojiwa na shirika la habari la Uingereza la bbc aliulizwa ikiwa hatua ya kuwalenga wapiga kura katika mtandao huo wa kijamii huenda inaweza kuwa chachu ya kubadili dira ya uchaguzi alijibu kwamba binafsi hafikirii kama hicho ni kweli na kimsingi katika suala la Marekani ni hatua ambayo ingeiharibu kabisa kampeini ya Trump badala ya kumsaidia. Kampuni ya Cambridge Analytica inadaiwa kwamba ilijaribu kushawishi mitizamo ya wamarekani kumuunga mkono Donald Trump.

Mtandao wa kijamii wa Facebook umekumbwa wiki hii na sakata la lililofichuliwa na  Christopher Wylie anayesema kwamba kampuni hiyo ya Cambridge Analytica ya Uingereza ilipewa kazi na Trump ya kumsaidia katika kampeini yake mwaka 2016 na kutumia  njia zisizohalali kupata taarifa za watumiaji millioni 50 wa mtandao wa Facebook.

Großbritannien Dr Aleksandr Kogan Lehrkraft University of Cambridge
Dr Aleksander KoganPicha: University of Cambridge

Facebook imepoteza thamani ya billioni 60 katika soko lake la hisa katika kipindi cha siku mbili zilizopita  kufuatia khofu iliyotanda kwamba mahusiano yake na Cambridge Analytica huenda yakaiharibia sifa. Hata hivyo Facebook inasema kwamba data zilizotumika zilikusanywa na Aleksandr Kogan msomi wa soshologia aliyeunda App maalum katika jukwaa hilo la Facebook ambayo iliyopakuliwa na watu 270,000. Facebook lakini inasema kwamba baadae Kogan alikiuka sera za mtandao huo kwa kuzisambaza data hizo kwa kampuni ya utafiti ya Cambridge Analytica.Mfichuzi wa sakata hili Christopher Wylie akizungumzia zaidi anachokifahamu alisema

''Kile ninachokisema kinatokana na maarifa niliyonayo katika kampuni na kwa kufahamu kile ambacho tulikuwa tukikitafuta. Kwa uwazi kabisa nadhani kwamba kile ambacho tulikuwa tunakitengeneza hapana shaka kabisa  kingeweza kuwa na athari kubwa katika chaguzi.Lakini kwangu mimi ni vigumu sana kutenganisha kigezo kimoja juu ya kingine''

Kogan anayedaiwa kutengeneza App iliyokuja kutumiwa kuzikusanya data za watu kinyume na sheria anasema kwa ulewa wake walihakikishiwa na kampuni ya Cambridge Analytica kwamba kila kitu kiko katika misingi ya sheria na ndani ya muongozo na kanuni za kampuni hiyo. Alexander Nix ambaye ni mkuu wa Cambridge Analytica aliyetimuliwa jana ,kupitia vidio iliyorekodiwa kwa siri amesema kwamba Kampuni hiyo ilibeba dhima muhimu katika ushindi wa Trump kwenye uchaguzi uliopita nchini Marekani.Kisa hiki kimewafanya pia maafisa wa Umoja wa Ulaya kutoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa haraka wakati wabunge nchini Uingereza wakimtaka mmiliki wa Facebook Zuckerberg kutoa ushahidi mbele ya kamati kuu ya bunge la Uingereza.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo