FA: Arsenal yaizamisha Manchester City | Michezo | DW | 24.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

FA: Arsenal yaizamisha Manchester City

Arsene Wenger amekiri kuwa ushindi wao wa kujituma wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester City ulikuwa ahueni kubwa kwa sababu ilidhihirisha kuwa wachezaji wake wanaweza kufanya vyema chini ya shinikizo kubwa

Arsenal walishinda mechi hiyo ya Wembley 2-1 katika muda wa ziada na kujikatika tikiti ya kupambana na vinara wa Ligi ya Premier Chelsea mnamo Mei 27. Chelsea waliwazaba Tottenham Hotspurs 4-2. Huenda ushindi wa ARsnal umempa kidogo Wenger fursa ya kupumua kutokana na miito ya kumtaka ajiuzulu.

Baada ya kichapo hicho kumwacha Mhispania huyo bila nafasi ya kutwaa taji lolote kwa mara ya kwanza katika taaluma yake yenye mafanikio makubwa zaidi, Pep Guardiola anasisitiza kuwa Manchester City itakuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao. Amesema msimu huu ulikuwa wa kujifunza na atakifanyia mabadiliko kikosi chake tayari kwa msimu ujao.

Kante mchezaji bora wa mwaka England

Wakati huo huo, kiungo wa Chelsea N'Golo Kante ameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Chama cha Wacheza Kandanda la Kulipwa katika msimu wa 2016 – 17. Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 26 alimpiku mwenzake wa Chelsea Eden Hazard, Harry Kane wa Spurs, Zlatan Ibrahimovic wa Manchester United, Romelu Lukaku wa Everton na Alexis Sanchez wa Arsenal. "Ni kitu cha maana sana kwangu kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka. ni muhimu sana katika misimu hii miwili. Mmoja na Leicester na tuko katika hali nzuri na Chelsea na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka ni heshima kubwa". Alisema Kante.

Amecheza kuanzia mwanzo mechi zote za Chelsea kwenye ligi isipokuwa moja tu mwaka huu. kiungo wa Spurs Delle Alli alishinda kwa msimu wa pili mfululizo tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka.

Na Alli ameisaidia sana Spurs kupunguza pengo kati yao na Vinara Chelsea hadi pointi nne tu hali ambayo imekiweka wazi kinyanyang'anyiro cha ubingwa wa England ikiwa imesalia mechi sita tu. Chelsea watacheza dhidi ya Southampton kesho usiku.

Tottenham watakuwa na mtihani mkali dhidi ya Crystal Palace siku ya Jumatano. Kinyang'anyiro cha kucheza Champions League pia kitapamba moto katika debi ya Manchester siku ya Alhamisi. Nambari nne Manchester City watakutana na Manchester United ambao wako nyuma yao na pengo la pointi moja tu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com