Evo Morales asema yuko tayari kurejea Bolivia iwapo raia wanamtaka kufanya hivyo. | NRS-Import | DW | 14.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Evo Morales asema yuko tayari kurejea Bolivia iwapo raia wanamtaka kufanya hivyo.

Aliyekuwa rais wa Bolivia Evo Morales aliye uhamishoni Mexico, amesema kuwa yuko tayari kurejea nchini mwake ''haraka iwezekanavyo'' huku wafuasi wake wakikabiliana na polisi katika maandamano dhidi ya Jeanine Anez .

Akiongea na waandishi habari mjini Mexico City, Morales alitoa wito wa mashauriano kati ya pande zote na kusema " Bila shaka nitarejea nchini Bolivia watu wangu wakitaka nifanye hivyo kutuliza hali ilivyo nchini humo lakini mashauriano ya kitaifa ni muhimu. Nadhani bila mashauriano ya kitaifa - naona itakuwa vigumu kusitisha mapigano haya."

Watu wawili wamekufa katika mapigano kati ya wafuasi wa Morales na wale wanayoiunga mkono serikali ya mpito pamoja na vikosi vya usalama. Hii inafikisha idadi ya waliokufa katika maandamano ambayo yamedumu kwa wiki tatu kufikia watu 10.Shirika la habari la Todo Noticias limeripoti kuwa maafisa wa polisi walifyatua gesi za kutoa machozi siku ya Jumatano huku waandamanaji waliotaka kurejeshwa mamlakani kwa Morales wakikabiliana nao.

Jumba moja limetekezwa katika mji jirani wa El Alto. Maandamano pia yameripotiwa katika maeneo ya Cochabamba na Chuquisaca katika maeneo ya Kati na Kusini mwa nchi. Siku moja baada ya Jeanine Anez kuchukuwa hatamu za uongozi, mapigano makali yalizuka kati ya wafuasi wa Morales na polisi wa kukabiliana na ghasia. Upinzani pia uliibuka bungeni ambapo wabunge wanaomuunga mkono Morales waliweka shinikizo za kupinga uhalali wa wadhifa huo mpya wa Anez kwa kujaribu kuandaa vikao vipya vya bunge ambavyo vingehujumu wadhifa huo mpya wa urais.

Vikao hivyo vilivyopuuziliwa mbali kuwa kinyume cha sheria na upande unaomuunga mkono Anez vimeongezea hali ya sintofahamu ya kisiasa kufuatia kujiuzulu kwa Morales siku ya Jumapili kufuatia wiki kadhaa za maandamano dhidi ya madai ya uchaguzi uliokumba na mizengwe uliofanyika Oktoba 20 ambapo rais huyo alidai ushindi wa moja kwa moja dhidi ya mpinzani wake wa chama kinachoegemea siasa za mrengo wa kulia Carlos Mesa.

Morales ambaye ni kiongozi wa kwanza kutoka jamii asilia ya taifa hilo na aliyekuwa madarakani kwa takriban miaka 14 alikimbilia uhamishoni siku ya Jumanne na kuchangia naibu rais wa baraza la seneti Jeanine Anez kujitangaza kuwa kaimu rais. Mkosoaji huyo wa Morales wa umri wa miaka 52 alisema kuwa katiba inamruhusu kuchukuwa hatua hiyo baada ya rais, naibu wake na maspika wa mabaraza yote mawili ya bunge kujiuzulu.

Morales anadai kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria kwa kuwa bunge la Bolivia bado halijaidhinisha hatua ya kujiuzulu kwake.Katika mahojiano na gazeti la El Pais mjini Mexico City, Morales alisema kuwa iwapo bunge halijaridhia kujiuzulu kwake, yeye bado ndiye rais.