1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Europol : Uhalifu dhidi ya watoto mitandaoni waongezeka

Saleh Mwanamilongo
29 Desemba 2020

Mkuu wa shirika la polisi la Ulaya amesema visa vya uhalifu wa kuwadhalilisha watoto kingono mitandaoni vinaongezeka kwa kipindi hiki cha janga la Corona.

https://p.dw.com/p/3nKfA
Europol I Razzia gegen einen mutmaßlichen Drogenring in Brasilien, Europa und Asien
Picha: Europol

Mkuu wa shirika la polisi la Ulaya, Catherine De Bolle, amesema visa vya uhalifu wa kuwadhalilisha watoto kingono mitandaoni vinaongezeka kwa kipindi hiki cha vizuizi kutokana na janga la Corona. Akiita hali hiyo kuwa ni ya hatari.

Ripoti iliyochapishwa na shirika la polisi la Ulaya, Europol, inasema washukiwa wanajaribu kuwasiliana na watoto wanaotumia mda mrefu mitandaoni wakati wa vizuizi vya kubaki manyumbani.

Mkuu wa shirika la Europol amesema visa vya uhalifu wa kingono dhini ya watoto vinaongezeka mwaka huu kutokana na janga la Corona.

Chatherine De Bolle ameliambia gazeti la Ujerumani la Funke kwamba hali hiyo inaleta wasiwasi kutokana na kwamba ongezeko la visa hivyo ni kubwa zaidi kuliko kipindi cha kabla ya janga la corona.

De Bolle amesema wameshuhudia ongezeko la kasi la uhalifu wa mitandaoni na ni jambo la hatari.

Ujerumani yawasaka washukiwa 

Mkuu wa shirika la polisi ya Ulaya,Europol, Chatherine De Bolle.
Mkuu wa shirika la polisi ya Ulaya,Europol, Chatherine De Bolle.Picha: picture-alliance/dpa/T. Roge

Mkuu huyo wa shirika la kupambana na uhalifu la Umoja wa Ulaya amesema mara nyingi  wahalifu wamejaribu kuwasiliana moja kwa moja na watoto waliokuwa mitandaoni kwa mda mrefu kuliko kawaida na ambao hawatizamwi.

Shirika la Europol lenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi, linasaidia nchi 27 za Umoja wa Ulaya katika vita vyake dhidi ya ugaidi,uhalifu wa mtandaoni na aina nyingine ya visa vya uhalifu wa kupangwa.

Mapema mwezi huu wachunguzi kwenye jimbo la North Rhine-Westphalia ,hapa nchini Ujerumani, waliendesha kamatakamata dhidi ya washukiwa waliokutwa na picha na video za unyanyasasi wa watoto.

Waendesha mashtaka waliwalenga washukiwa 56 ,na kukamata data zaidi ya 330 zilizohifadhiwa kwenye vifaa tofauti.

Oktoba, serikali ya Kansela Angela Merkel iliidhinisha sheria mpya kuhusu visa vya udhalilishaji wa kingono dhidi ya watoto,ambayo inatoa adhadu ya hadi miaka 15 jela.

Kwa mujibu wa takwimu za uhalifu nchini Ujerumani ni kwamba mwaka 2019 kulikuwa na visa 25,000 vya udhalilishaji watoto na zaidi ya visa 12,000 vya uchunguzi dhidi ya uhalifu wa matumizi ya picha za watoto.

Ikiwa ni ongezeko la asilimia 65 ukilinganisha na mwaka wa 2018.

Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya watoto vimeendelea kuripotiwa kote ulimwenguni licha ya kuwepo kwa matamko na sheria kuhusiana na haki zao,kwani wakitendewa vibaya udogoni, maisha yao yanaharibika moja kwa moja.